Header Ads

TID Pokea Ushauri, Rudi Kwenye Fani ya Utangazaji


Nilianza kumfahamu msanii Khaleed Mohammed au Top in Dar (TID) alipotoa wimbo pendwa wa Zeze miaka ile ya 2000s akiwa na Jay Moe..

Jina lake likakua na kukubalika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania huku akijivunia sauti yake na kujiita 'Golden Voice' yaani Sauti ya Dhahabu, jina ambalo alilipa album yake ya kwanza iliyojaa nyimbo zilizobamba tupu kwa wakati huo..

Kuna kituo maarufu cha redio, kiliwahi kutumia sauti yake kufanyia 'jingle' matata sana kwa miaka mingi kabla TCRA haijabadili 'masafa' kwa vituo vya redio zote nchini. Ile Jingle ni shida (92.9, Magic Fm, Dar es salaam)..

Historia tamu ya SAUTI YA DHAHABU ninayo, ila kwa leo acha niishie hapo.

Kucheza? Nani hakumbuki 'shekisheki' za TID zilivyovuruga vijana mitaani kwetu? Kuna aliyesahau kwamba TID ndiye msanii pekee aliyebuni michezo mingi ya kuvunja (breakdance) hapa Bongo, kiasi cha kupachikwa jina la 'Wacko Jacko', likimaanisha 'Michael Jackson', jina la mfalme wa muziki wa Pop na 'michezo ya kuvunja' duniani (apumzike kwa amani).

Jina la TID liliuza magazeti, lilivuta mapromota (mameneja waliitwa mapromota wakati huo), lilileta hamasa ya vipindi vya muziki kwenye televisheni zetu nchini.. Alitamba kila siku.. Alikuwa NEMBO ya muziki wa kizazi kipya..

TID alijua kuimba na kucheza. Andaa show, usimuite TID, imekula kwako! Inakadiriwa kuwa ndiye mwanamuziki wa kwanza kwenda kufanya ziara ya kimuziki Uingereza. Yes, wa kwanza kutoka Bongoflevani. Huko akafyatua na video ya wimbo wake wa 'Pekee'. Wapo waliokoma kwa hili!

Sijasahau, umaarufu wa TID ndio uliibeba filamu bora ya maisha na muziki kuwahi kutokea hapa nchini, Girlfriend, akiwa kama mhusika mkuu akishirikiana na dada Monalisa wa Natasha. Hata leo hii, tunakubaliana kwamba hapakuwahi kutokea filamu ya Kiswahili iliyotazamwa na kukubalika nchini zaidi ya hiyo. Kila mtu alimwangalia zaidi TID humo. Mungu ampumzishe kwa amani mtayarishaji George Tyson.

Hayo yamepita.

Kuna fani TID aliyosomea. Fani ya Utangazaji. Sio kusomea tu, huko ndiko alikotokea kabla ya kuingia kwenye muziki. Wengi hawakulijua hili la utangazaji mpk pale jina lake lilipokuwa kubwa kupitia muzikia.. Mimi nikiwa mmojawapo. Kama kuna ambaye halijui hilo, habari imfikie rasmi leo.

Ngoja nikueleze, TID alikuwa anasifika kwa umahiri wa kutangaza redioni. Hakuwa maarufu kwa sana, lakini alikuwa hodari na machachari sana akiwa nyuma ya maiki. Sifa yake kubwa ilikuwa ni sauti ya bashasha na umahiri wa kutumia lugha ya kiingereza 'kimjini mjini'. Acha bwana! Ulikuwa ukimsikiliza TID siku za weekend usiku, hata kama ulikuwa na mpango wa kwenda club utaghairi. Taji Liundi heshima kwako kwa kukivumbua hiki kipaji..

Sina data nyingi kuhusu 'utangazaji' wa TID, lakini naamini ni kitu anachoweza kufanya zaidi na kukubalika hasa katika kipindi hiki ambacho muziki una 'vurugu' na fitina za kutosha.

Hapa namuwazia Mtangazaji TID mwenye makeke lakini yasiyo na utani utani. Namjengea picha akiwa ni mtangazaji anayeheshimu wasikilizaji wake na mwenye nidhamu ya kazi.

Nani asingependa kumsikiliza TID nyakati za jioni? Rudi kazini TIDI.

By Interest

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.