Header Ads

SABABU Zilizofanya Waziri Mkuu wa Zamani Fredrick Sumaye Kunyang'anywa Shamba lake


Hatimaye shamba lililokuwa linamilikiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, lililopo Mabwepande limefutiwa hati zake na umiliki umerudishwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo itafanya utaratibu wa kupima viwanja na kuwagawia wananchi waliohusika kwenye mgogoro huo.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi zaidi ya 250 kulalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa kupitia shamba hilo, na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Hapi kupeleka malalamiko hayo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo Rais John Magufuli aliidhinisha kufutiwa hati kwa shamba hilo.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo ya Mabwepande jana, Hapi alisema shamba hilo lenye ekari 33 limefutiwa hati zake tangu Oktoba 28, mwaka huu na kwamba tayari Sumaye ameandikiwa barua ya kutojihusisha na shamba hilo baada ya kushindwa kukidhi masharti ya kisheria.

“Vyombo vya ulinzi na usalama watakuwepo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shamba hili halitafanyiwa shughuli zozote isipokuwa baada ya taratibu za Manispaa zitakapofanyika,” alisema Hapi na kuongeza;

“Mgogoro wa shamba hili ni wa muda mrefu uliowahusisha wananchi. Lakini tunayo idadi ya wananchi ambao walikuwepo kwenye huu mgogoro na sasa wataalamu wataandaa mpango bora wa matumizi ya shamba hili,” alisema.

Aliongeza kuwa, wananchi hao waliokuwamo kwenye mgogoro ambao wataonekana wana vigezo vya kupatiwa viwanja, watafikiriwa kwa masharti ambapo baada ya kupimwa viwanja hivyo watawekewa gharama nafuu kwa ajili ya wao kununua.

Pia alisema, wananchi hao wenye makazi ya kudumu kwenye eneo hilo, watahakikiwa ili kuepusha watu wasiokuwamo kujiingiza kwa lengo la kuonekana nao walikuwa sehemu ya tukio.

Hata hivyo, alisema wataendelea kutoa taarifa kwa Rais kuhusu maeneo ambayo wananchi wanayahodhi bila ya kuyafanyia kitu chochote ili nayo yafutiwe hati.

“Natoa rai kwa wananchi wengine wenye maeneo ambayo hawayaendelezi tutayafutia hati na tutayamiliki wenyewe Manispaa ya Kinondoni. Pia tuendee kumuombea kwa kazi zake nzuri ili Mungu ampe ujasiri wa kupambana na ukabaila unaofanywa na wanaohodhi rasilimali za umma,” aliongeza.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Aaron Kagurumjuli kwa upande wake alisema, watahakikisha hadi Alhamisi wiki ijayo, timu ya ardhi wanaanza kupima viwanja hivyo na kuwagawia wananchi kwa masharti watakayoweka.

Kagurumjuli alisema watakaopewa kipaumbele katika ugawaji wa viwanja hivyo ni wale wenye makazi ya kudumu na watu ambao hawana makazi ya aina hiyo, watafikiriwa.

Wakazi wa kata hiyo walimpongeza Rais kwa hatua hiyo na kueleza kuwa matatizo kama hayo yapo sehemu nyingi nchini na yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.

Abdallah Mohammed alisema kuwa walikuwa wanapata mateso kutoka kwa baadhi ya maaskari ambao walikuwa wanawanyanyasa kwa kuwatoa majumbani mwao usiku wa manane na kuwafungulia kesi.

Happy Makole alisema walikuwa wanaishi kwa wasiwasi kwa kuwa askari walikuwa wanawakamata waume zao na kuwaacha peke yao.

“Tumenyanyasika sana kuhusu eneo hili, mimi niliachwa usiku wa manane nikiwa na mtoto wakati mume wangu alipokuja kukamatwa. Lakini pia yapo maeneo mengine tunaendelea kunyanyasika tunaomba wayafanyie kazi malalamiko yetu,” alisisitiza Makole.

 – HABARILEO

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.