Header Ads

KWA Hili Lady Jaydee na Clouds Media Group Wanastahili Pongezi


Najua hakuna aliyetarajia kuona hili likitokea lakini kwa uwezo wa Mungu limefikia mwisho.

Nakumbuka Machi 21 ya mwaka huu kaka yangu Fredrick Bundala aliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “Ninachotamani: Lady Jaydee na Clouds Media Group wamalize tofauti zao” hatimaye hilo limesikika na kila kitu kimeonekana kuwa sawa kutokana na pande zote mbili kuamua kufukia mabaya yote yale yaliyowahi kutokea.

Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, napenda kumpongeza Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kwa busara yake aliyoitumia ya kujibu swali aliloulizwa kwenye kipindi cha XXL kuhusu kumaliza ugomvi wao na malkia wa muziki wa Bongo Fleva, Jaydee.

“Tatizo ni kwamba hakuna ambacho hatujamaliza, tulimaliza, tunasubiri order. Unajua kimsingi ulipopewa order ya kwamba ‘nyimbo zangu usipige, jina langu usiseme kwenye chombo chako, vyovyote itakavyokuwa mimi sitaki kusikia hiyo kitu’ hiyo ndio order. Kwahiyo labda tukikutana, nimuombe tena [Lady Jaydee] kama tutaruhusiwa kufanya hiyo kitu,” alisema Ruge kwenye kipindi hicho.

Aliongeza kwa kusema kuwa ni muda mrefu hajawahi kukutana na Lady Jaydee, japo alidai ‘hata leo nikipata nafasi ya kahawa nitashukuru sana kwa huo mwaliko.’

Hatimaye ujumbe ule ulimfikia Jaydee na nampongeza hakutaka kuliacha jambo hilo lipite kwa kuwa limedumu kwa muda mrefu na hakuna jipya lililotokea kwa kuwa kila mtu bado anafanya kazi zake huku mashabiki ndio wakibaki njia panda wakishindwa cha kufanya.

Jumatano hii uongozi wa Jide ulitoa taarifa yake rasmi kuwa wapo tayari kufanya kazi tena na kituo hicho cha redio. “Hatuna tatizo na Clouds Media Group kuanza kupiga nyimbo za Lady Jaydee. Wanaweza kuanza kupiga wakati wowote watakapokuwa tayari kwakuwa chochote kilichotokea hapo nyuma kimefikia tamati, la msingi sasa ni amani na upendo vitawale. Kuanzia leo wana uhuru wa kupiga na kutaja jina la Lady Jaydee kadri wawezavyo,” yalisema maelezo yake.

Kitendo hicho kilichofanywa na pande zote mbili kitawarudisha upya tena baadhi ya mashabiki waliogawana upande pamoja na kuwapa nafasi wasanii ambao walikuwa wakitamani kufanya kazi na Jide kwa muda mrefu lakini walikuwa wakihofia nyimbo zao kutochezwa kwenye kituo hicho.

Kama hili limewezekana basi natamani pia kuona siku moja wasanii wengine ambao hawapatani na kituo hicho na vituo vingine vya habari wakiyamaliza matatizo yao na kuendelea kuufanya muziki wetu kusonga mbele kwa kuwa wote tupo kwenye safari moja na kila mtu anamtegemea mwenzake ili kuhakikisha hilo linatimia.

By Salum Kaorata

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.