Header Ads

ZITO KABWE ACHOCHORA, ASAKWA NA POLISI USIKU NA MCHANA.

KIONGOZI Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amekimbilia nje ya nchi baada ya kunusurika kukamatwa na Polisi alipokuwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,.

Kiongozi huyo alikuwa amekwenda mkoani Geita na Kahama kwa ajili ya kufunga kampeni za udiwani kwa ajili ya wagombea wa chama chake lakini hajaonekana hadharani hapa nchini tangu Januari 22 mwaka huu (Jumapili iliyopita).

Ingawa hakuna kiongozi wa ACT-Wazalendo wala mwanafamilia aliyekuwa tayari kueleza wapi alipo mbunge huyo wa Kigoma Mjini,lakini taarifa zinadai kwamba Zitto alitorokea nje ya nchi.

Jumapili iliyopita, chama cha ACT-Wazalendo kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyoeleza kwamba kulikuwa na kusudio la kumkamata Zitto mara baada ya kumaliza mikutano ya kufungia kampeni za udiwani uliofanyika wiki iliyopita.

Polisi haijaeleza sababu hasa za kutaka kukamatwa kwa Zitto, lakini taarifa hiyo ya ACT-Wazalendo kwa wanahabari ilieleza kwamba kiongozi wao huyo alikuwa akitafutwa kwa madai ya uchochezi.

Lakini, wiki tatu zilizopita, mwanasiasa huyo alizungumza mjini Kahama ambapo pamoja na mambo mengine, alimshutumu Rais John Magufuli kwa kauli zisizo za kiungwana alipokuwa mkoani Kagera kuwapa pole wahanga wa tetemeko la ardhi.

Siku moja baada ya kauli hizo za Zitto ambazo zilizasambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo rasmi vya habari, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu, alinukulia na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba wanasiasa watakaokashifu viongozi wa kitaifa wakati wa mikutano ya kampeni wilayani kwake watakamatwa.

" Kuna viongozi walikuwa wanaheshimika sana lakini naona siku hizi wameishiwa. Badala ya kuzungumzia kero za wananchi wao wanakashifu viongozi wa kitaifa. Hili halivumiliwa tena wilayani kwangu," Nkurlu alinukuliwa akisema.

Katika mkutano wa mwisho wa ACT uliofanyika katika Kata ya Isagehe wilayani Kahama, kulikuwa na idadi kubwa ya askari pamoja na magari ya kulinda usalama kuliko ilivyokuwa kawaida.

Mmoja wa viongozi wa juu wa ACT-Wazalendo aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina, alisema walipata taarifa za kishushushu kwamba kiongozi wao atakamatwa baada ya mkutano huo.

" Sisi tuliambiwa kwamba magari yale yanamsubiri Zitto ashuke ili akamatwe. Nasi pia tuna vyanzo vyetu. 
Tulichofanya ni kuhakikisha KC (Kiongozi wa Mkuu wa Chama) anashuka kwa haraka na njia za kijasusi ili asikamatwe. Tunashukuru kwamba tulifanikiwa kwenye hilo," alisema kiongozi huyo machachari.

Habari ambazo Raia Mwema imezipata zinaeleza kuwa Zitto aliondoka Kahama kwa kubadili magari usiku kucha na aliondoka nchini kupitia mpaka wa Manyovu, mkoani Kigoma.

Vyanzo vya gazeti hili vimeeleza kwamba viongozi wa chama waliona kwamba kama angekamatwa siku ya Jumamosi, maana yake ni kwamba angekaa rumande hadi Jumatatu na kusingekuwa na uhakika wa kutoka siku hiyo.

" Kama unafuatilia suala la mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, utabaini kwamba serikali ikiamua unaweza kukaa ndani kwa muda inaotaka. Ndiyo maana tukaona busara ni kuondoka ili asikamatwe," gazeti hili limeelezwa.

Katika mazungumzo ambayo Zitto mwenyewe amedaiwa kuyafanya na baadhi ya wandani wake kwenye familia yake, inadaiwa alieleza kuwa amepewa tahadhari na watu anaowaamini kuwa serikali inapanga kumkamata na kumfungulia mashtaka ambayo yatamfanya afungwe kifungo kirefu ili apoteze sifa ya kuwa mbunge na kugombea urais kwenye chaguzi zijazo.

Watu walio karibu na mwanasiasa, wanadai kwamba Zitto alikuwa akipuuza tahadhari hizo mpaka pale alipopewa ujumbe maalumu na rafiki zake walio serikalini kuwa imepangwa akamatwe na atakamatwa ama Geita au Kahama.

Walipoulizwa  wapi alipo kiongozi wao huyo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa na mshauri wa chama hicho, Kitila Mkumbo, walikana kuwa Zitto yu nje ya nchi, lakini hawakuwa tayari kusema alipo hapa nchini.

" Nani kakwambia Zitto yuko nje ya nchi? Mimi najua kwamba yupo na yupo salama. Hizo habari kwamba hayupo Tanzania ni mpya kwangu. Labda nizifuatilie muda huu," alisema Kitila, ambaye ni mmoja wa wasomi maarufu nchini.

Katika siku za karibuni, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakiwamo wabunge wameingia matatani na vyombo vya dola kutokana na matamshi na vitendo vyao walivyovifanya.

Viongozi wa karibuni zaidi kuingia katika mkono wa dola ni Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Selemani Mathew na Katibu wa Chadema Kijiji cha Nyangamara ‘A’ mjini Lindi, ambao wamehukumiwa kifungo cha miezi minane jela bila ya faini kutokana kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi katika kijiji hicho wilayani Lindi.

Viongozi hao waliohukumiwa ni kati ya viongozi sita waliokamatwa na kutuhumiwa kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi nchini.

Viongozi hao walidaiwa kufanya mkutano huo wa hadhara mnamo Aprili 3, mwaka jana  bila ya kibali cha Jeshi la Polisi wilayani Lindi.

Selemani Mathew aliwahi kuwa Diwani wa Vijibweni wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya CCM. Aligombea katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi mwaka juzi, ambapo katika kura za maoni za CCM alishindwa na Nape Nnauye.

Baadaye alihamia Chadema ambako alikuwa mgombea ubunge wa chama hicho, lakini pia alishindwa na Nape ambaye sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Pia, mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, naye anatumikia kifungo cha miezi sita jela kwa madai ya kufanya fujo katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mwaka jana.

Kwa upande wake, Lema yuko rumande kwa takribani miezi miwili sasa, kwa madai ya kutoa kauli za kashfa dhidi ya viongozi.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.