Header Ads

KAMBI ya Upinzania Bungeni Yamlima Barua IGP Mangu..Ni Kuhusu Vurugu za Lipumba Cuf..!!!


KAMBI ya Upinzani bungeni imemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu na taasisi za Serikali kuhoji tukio la mkutano wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoa wa Dar es Salaam kuvamiwa na watu wenye silaha juzi.
Watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba walivamia mkutano wa mwenyekiti wa mkoa na wanahabari wakiwa na bastola, fimbo na mikanda na kutishia maisha, kupiga watu waliokuwa kwenye ukumbi wa hoteli moja jijini na kufanya virugu.
Aidha, upinzani umemtupia lawana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kuhusu uvamizi huo kwa kuwa hawakutekeleza majukumu yao.
Kadhalika, umelaani kitendo hicho cha uvamizi wa mkutano pamoja na waandishi wa habari kupigwa kwa kuitaka Serikali kutoa tamko na kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.
Mnadhimu wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni wa CUF, Ally Saleh akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema makundi ya uvamizi yamekuwa tishio katika jamii.
“CUF kimeshamwandikia barua IGP na taasisi zinginezo za Serikali kuonyesha matatizo yaliyotokea jana (juzi) na chanzo cha matatizo hayo," alisema Saleh. "Tunangojea Serikali itasema nini juu ya tukio lile.”
Saleh ambaye pia ni Naibu mnadhimu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bungeni, alisema kitendo kilichotokea katika mkutano wa CUF cha watu kuvamia na kutoa bastola hadharani hakina utofauti na tukio alilofanyiwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Alisema ukimya wa Waziri Mwigulu na Dk. Mwakyembe juu ya tukio hilo umeonyesha hawajatimiza majukumu yao; hususani Waziri Mwakyembe ambaye alipaswa kuhakikisha waandishi wa habari wanakuwa salama.
“Mambo haya yanavyotokea mawaziri wawili tunataka kuwavisha mnyororo Waziri Mwigulu Nchemba na Mwakyembe," alisema.
"Mwakyembe alipaswa kujitokeza kwa haraka na kutoa tamko dhidi ya kitendo walichofanyiwa waandishi, tunahisi kwamba jukumu a Serikali halijatekelezwa, Mwakyembe anapaswa kuhakikisha usalama wa waandishi unakuwapo. Hivyo Mawaziri hawa wawili wanapaswa kutoa tamko."
Alisema kikundi cha Mungiki siyo kigeni hapa nchini na Serikali inakifahamu lakini hakuna hatua zozote ambazo zimeshachukuliwa hadi sasa.
Kadhalika, alisema Kutokana na tukio lililotokea juzi, mkutano wa ndani wa kikatiba uliotakiwa kufanywa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad leo Serikali wameufuta kitendo ambacho siyo sahihi.
Alisema kitendo cha Serikali kuufuta mkutano huo siyo sawa kwa sababu Profesa Lipumba anabebwa na mbereko ya Serikali kwa kufanya mikutano ya ndani kila wakati.
Alisema Serikali inalea Jamhuri ndogo ndani ya Jamhuri, vile vile Serikali imekuwa inalea kambi ndogo ndani ya Buguruni na kwamba wanufaika zaidi wa mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao dhumuni lao ni kuchukua majimbo yanayoongozwa na CUF katika uchaguzi mkuu ujao.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.