Header Ads

Mbowe Naye Avunja Ukimya..Ampa Makavu Live Rais Magufuli ..Afunguka Jini Wapinzani Wanavyoteswa na Kunyanyaswa na Serikali..!!!!

KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe amesema mwaka mmoja na nusu wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano umekuwa ni wa manyanyaso na uonevu kwa baadhi ya viongozi na watendaji wao kuuwawa au kupotea na Serikali ikiwa kimya.
Mbowe aliyasema hayo katika hotuba ya kambi hiyo bungeni kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, mwishoni mwa wiki ambapo alitolea mfano mauaji na kesi zinazowakumba wapinzani kila kukicha.
Alisema katika kipindi hicho wameshuhudia mauji ya wanachama, kutekwa, kukamatwa kwa wabunge na wanachama na kesi mbalimbali ambazo hazina msingi zikiwa na lengo la kuwakatisha tamaa.
Alitolea mfano kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo na kusema aliuawa mchana kweupe, huku watu wakishuhudia na kwamba waliohusika wanajulikana, lakini hakuna hatua ambazo zilichukuliwa.
“Msaidizi wangu Ben Saanane alipotea baada ya kupokea vitisho kadhaa vyenye asili ya kisiasa na hadi sasa vyombo vya dola havijatoa maelezo ya kina ya Ben kapelekwa wapi,” alisema.
Mbowe alisema pamoja na changamoto hizo, Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa upande wao na hila hizo za baadhi ya wenye mamlaka, hazijawaondoa kwenye lengo kubwa la kuwavusha wananchi wa Tanzania kuifikia ndoto zao.
Alisema wabunge wa upinzani hawajawa salama kwa kile alichodai kuwa kifungo cha Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali kilikuwa cha uonevu mkubwa na Mbunge wa Arusha Godbless Lema kunyimwa dhamana kwa zaidi ya miezi minne kwa shtaka lenye dhamana.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema katika kipindi hicho pia wameshuhudia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akikamatwa mara kwa mara na vyombo vya dola na kufunguliwa mashtaka mbalimbali yasiyo na nia njema wala afya kwa ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu.
“Tunaamini mapito haya mazito ya kisiasa katika nchi yetu yanalenga kujaribu kufifisha ndoto ya Taifa   ndoto ya kuwa taifa huru linalosimamia misingi ya haki za binadamu, uhuru wa maoni ya kila raia, demokrasia ya kweli, kuwa taifa linaloheshimu Katiba ya Nchi na taifa lenye uchumi unaomnufaisha kila mwananchi,” alisema.
Mbowe alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, zimeonekana dalili za wazi za Serikali hiyo kuvunja Katiba ya Nchi kwa kutupilia mbali misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa kupata habari jambo ambalo linaweza kuitumbukiza nchi yetu kwenye dola la ki- dikteta.
Alibainisha matukio mahsusi ya ukandamizaji wa haki na demokrasia yaliyofanywa na serikali kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kuwa ni pamoja na kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa.
Serikali kupitia Waziri Mkuu na Rais, ilitangaza kwamba ni marufuku kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020 ili kuipa Serikali nafasi ya kufanya kazi.
”Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba aidha, katazo la mikutano ya siasa linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya 1992 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa Mijadala ya Bunge ni kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila mwananchi.
Alisema pia bungeni yamekuwapo matukio kadhaa yanayoashiria kutaka kuwadhibiti wabunge wa upinzani kwa lengo la kuwanyamazisha wasiikosoe Serikali.
Kiongozi huyo alisema jambo hilo limefanyika kwa namna mbalimbali, ikiwamo kuwazushia kesi wabunge wa upinzani na kuwapeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambako hukumu ya kuwaadhibu inakuwa imeshaandaliwa.
Alibainisha kuwa changamoto nyingine ni Serikali kuingilia muhimili wa Mahakama, kupuuza utawala wa Sheria, uonevu aliodai kufanywa na vyombo vya Dola dhidi ya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.