Header Ads

Ripoti ya CAG Kulitikisa Bunge..Wabunge Wapania Kuiadhibu Serikali Kutokana na Madudu Yaliyomo Kwenye Ripoti Hiyo..!!

BUNGE la Bajeti linaendelea leo Dodoma huku kukiwa na kila dalili za wabunge ‘kuwasha moto’, hali inayoweza kuibua mvutano mkali kutokana na ‘madudu’ yaliyotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Licha ya kuwa wiki hii kunatarajiwa bajeti ya Ofisi ya Rais na ya Makamu wa Rais zitawasilishwa, hilo haliwezi kuwaondoa wabunge katika mjadala wa ripoti hiyo ambayo Serikali haiwezi kukwepa kuwajibika kushughulikia yaliyotajwa.
Ripoti hiyo imeanika ‘madudu’ kila kona, huku deni la Taifa likizidi kupaa na kueleza namna vitendo vya ukwepaji kodi katika taasisi mbalimbali za Serikali ikiwamo migodi ya dhahabu ambayo haijalipa kodi kwa miaka 10.
Jambo la kwanza ni ushauri uliotolewa na Profesa Assad kuhusu bajeti iliyopita jinsi ilivyotekelezwa ambapo aliishauri Serikali kupanga bajeti inayoweza kuitekeleza, badala ya kupanga kiasi kikubwa ambacho hakina uhalisia.
CAG alitoa kauli hiyo huku takwimu za Wizara ya Fedha zikieleza kuwa hadi Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ni Sh trilioni 3.97 kati ya Sh trilioni 11.8 zilizopitishwa na Bunge Juni mwaka jana kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) alisema alisema wabunge wanapoteza muda kukaa bungeni Dodoma kujadili bajeti hiyo aliyodai ni kiini macho.
Kwa mujibu wa Zitto, bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17) imeonesha upungufu mkubwa katika utekelezaji na kwamba baada ya kupitia taarifa zilizowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango kwenye Kamati za Bunge za kisekta alibaini kuwa bajeti ya 2016/17 ilipaswa kuwa Sh trilioni 24.8 na si Sh trilioni 29 iliyowasilishwa na Serikali Juni mwaka jana.
Mbali na bajeti, jambo jingine linaloweza kuzua mjadala ni taarifa ya uchunguzi ya Mei, mwaka jana kubaini matumizi mabaya ya msamaha wa kodi wa Sh bilioni 3.46 ambao ulitolewa kwa walengwa wawili walioagiza magari 238. Magari hayo yalisajiliwa kwa majina tofauti na waliopewa msamaha huo.
Jambo lingine ni jinsi ukaguzi ulivyobaini lita 20,791,072 za mafuta yenye msamaha wa kodi wa Sh bilioni 10.17 kwa ajili ya mgodi wa Buzwagi kwa miezi 18 yalivyosafirishwa kwenda kampuni ya M/S Aggreko na mkandarasi msaidizi ambaye hakuwa mhusika katika msamaha huo.
Wakati sakata la vitambulisho vya Taifa likiwa linafukuta, kwenye ripoti ya CAG imebainishwa jinsi ukaguzi ulivyojiridhisha kuwa uongozi na watoa huduma na wazabuni walivyoshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya Taifa.
Mambo mengine yatakayotikisa chombo hicho cha kutunga sheria ni ucheleweshwaji wa fedha za michango ya hifadhi za jamii, Tanesco kupata hasara, kushuka kwa mapato ya uwekezaji kwa kiasi kikubwa kwenye mifuko ya pensheni ya NSSF, PPF, PSPF na LAPF.
Ushuru wa Sh bilioni 15 ulioyeyuka bandarini, malipo ya mishahara ya Sh bilioni 7.3 na makato ya kisheria ya Sh bilioni 2.5 yaliyofanyika kwa watumishi walioacha kazi au kufariki dunia , Serikali kutokarabati ofisi za balozi za Tanzania nje ya nchi sambamba na Tanesco kuwa mteja pekee anayetumia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.