Pedeshee Ndama Alipa Milioni 200 na Kuachiwa Huru kwa Dhamana
Baada ya kufanikiwa kulipa
faini ya milioni 200 hatimae jana mfanyabiashara , Ndama Shabani
Hussein, maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng’ombe amepata dhamana.
Ndama amepata dhamana baada ya kuwa
na wadhamini wawili na kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye
thamani zaidi ya shilingi milioni 600.
Wiki iliyopita Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu ilimtia hatiani Ndama na kumuhukumu kwenda jela miaka
mitano au kulipa faini ya milioni 200 baada ya kukiri shtaka la
kutakatisha USD 540,000.
Aidha mahakama hiyo iliyoketi chini
ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ilimsomea masharti ya dhamana mshtakiwa
huyo iwapo angefanikiwa kulipa kiasi hicho cha milioni 200 ili awe huru
katika mashtaka matano yanayoendelea kumkabili mahakamani hapo ambayo
upelelezi wake bado haujakamilika.
Katika masharti hayo, Ndama alitakiwa
kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na atoe fedha taslimu kiasi cha
USD 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya milioni 600 mahakamani hapo ama
mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha
Licha ya kupata dhamana, Ndama alirudishwa gerezani kukamilisha taratibu kabla ya kuachiwa huru.
Hukumu hiyo ya shtaka la sita la
kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili wa Serikali, Christopher
Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na kuyakubali maelezo ya
awali na maelezo yote yanayounda shtaka hilo la kutakatisha fedha,
akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,
Wakili Msigwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa amekubali shtaka la sita
la kutakatisha fedha na maelezo yanayounda shtaka hilo, hawana
kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya Ndama ila ni rai ya upande wa
mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu
cha 13(a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha.
No comments:
Post a Comment