Header Ads

Saida Karoli Kurudi Kwako Umejifunza Kitu?


Mwanamuziki wa Muziki wa Asili nchini, Saida Karoli.
Pongezi za dhati kwa ndugu zetu Waislamu kwa kumaliza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani vizuri. Ombi langu miezi yote tuishi maisha ya toba kama ilivyokuwa kwenye mfungo, kwani tunaweza.
Unapomzungumzia wanamuziki wa Muziki wa Asili, nchini ukiachana na Wanne Star, Sisi Tambala, na wengine wengi basi Saida Karoli naye yumo kutokana na tungo zake kujaa ala na maneno ya asili ya Kitanzania.
Kwa mtu ambaye anapenda muziki mzuri wenye ladha nzuri ya Kitanzania basi mwanamama Saida anayo, ladha hiyo nzuri na ya kipekee utaipata kwake.
Saida aliyewahi kutamba na nyimbo kadhaa kama Maria Salome almaarufu kama Chambua Kama Karanga, Kaisiki na Mpenzi Kizunguzungu, wimbo ambao binafsi unanikosha kwa namna ala za muziki zilivyopangiliwa.

Mwanamuziki Saida ni kama umerudi upya kwenye gemu, jambo ambalo hata mimi nimelifurahia, ila ujio wako mpya unanifanya nijaribu kujiuliza maswali ambayo nahitaji yakufikie, yakufikirishe na kukufanya uchukue hatua dhidi ya madhalimu wa muziki na maisha yako.
Dada yangu Saida ulipotea sana, hata mjini huku unaonekana tena kwa sababu hukuwa na mpya kama wasemavyo watoto wa mjini.
Nakumbuka mara ya mwisho kuwasiliana nawe ni kipindi kile ulipokuwa unafanya shoo f’lani hivi Masumbwe mkoani Shinyanga.
Umerudi kwenye gemu, sawa. Je, umejifunza nini maisha nje ya muziki?
Umegundua muziki wako wa awali ulifeli wapi, kushindwa kupata mafanikio kama wasanii wengine?
Kwa sasa umerudi na mikakati ipi ili uweze kufaidi kipaji chako?
Ujio wako mpya umejipangaje kukabiliana na wanyonyaji waliokutumia awali, na ulipochoka wakakutema kama Big G?
Wasiwasi wangu isije kuwa umeibuliwa tena kutoka mafichoni ili utumike kama zamani, kama itakuwa hivyo basi naamini athari na madhara ya awamu ya pili yatakuwa ni mabaya sana.
Najaribu kukushauri tu kama mdogo wako, kuwa dada Saida usikubali tena kutumika kwa ajili ya kuwafanya watu wanunue magari na kujenga nyumba nzuri wakati wewe unaishi kwenye nyumba ya kupanga na kutembelea Bajaj.
Usikubali kufanyishwa shoo kwa ajili ya kuuza sura tu wakati promota anaingiza pesa, usikubali kuuza sura kwenye mitandao ya kijamii wakati hakuna pesa unayoingiza.
Ni kweli mfumo mzima wa tasnia ya muziki Bongo bado una maruweruwe. Hakuna mpangilio na mgawanyo mzuri wa kazi na mapato ya wasanii, zaidi ya wajanja wenye mirija kufaidi peke yao.
Awamu hii, zungumza mapema na mdau anayekusimamia kuwa unahitaji mgawane asilimia ambazo zitakufanya uingize fedha siyo uwe mtu wa kujificha kwa sababu kazi unayofanya haiendani na maisha yako halisi.
Au Saida huwezi kuhoji masilahi yako kwa kuhofia hutasaidia, kutachezewa ngoma zako, hutapata shoo za hapa na pale.
Kama kuna mwanamuziki aliyepaswa kuwa tajiri basi dada Saida ulistahili, kila sehemu ngoma yako ya Chambua Kama Karanga ilikuwa ni Wimbo wa Taifa.
Ujio wako mpya umejifunza nini kwa mtoko wako wa zamani?
Umejipanga kuepukana kutumiwa kama daraja la mafanikio ya watu wengine?
Ni kweli cha kale ni dhahabu pamoja na kutemwa kama big g lakini leo umeonesha ubora na kipaji cha kweli ambacho Mungu amekujalia.
Saida dada yangu msimu huu usikubali kutumiwa kienyejienyeji bila makubaliano yatakayokufanya uendelee kuwa Saida Karoli.
Kataa kufa maskini Saida, kipaji ulichopewa na Mwenyezi Mungu ndiyo utajiri wako, ndiyo msingi wa maisha yako mazuri ndicho kinaweza kukufanya ukajenga nyumba na kuendesha magari mazuri.
BARUA NZITO: GABRIEL NG’OSHA | RISASI MCHANGANYIKO

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.