Header Ads

RAIS Magufuli Asitisha Utoaji wa Leseni za Uchimbaji Madini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha utoaji wa leseni mpya za uchimbaji halikadhalika leseni ambazo zimeisha muda wake.Soma taarifa kamili:

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Geita ambao walizuia msafara wake katika maeneo mbalimbali wakati akiwa njiani kuelekea Chato.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 4 Julai, 2017 amehitimisha ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili Mkoani Mwanza kwa kuzindua mradi wa Uboreshaji wa huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika kijiji cha Nyamazugo Wilayani Sengerema.

Mradi huo wa maji umetekelezwa chini ya mpango wa maji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi bilioni 22.4. Mradi wa Maji Safi mjini Sengerema ulioanza tangu mwaka 2011 unatarajiwa kuwahudumia wakazi 138,000 ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi huo, Mhe. Rais Dkt. Magufuli amesema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza tatizo la maji la muda mrefu kwa wakazi wa Sengerema na maeneo ya jirani.

Mhe. Rais Dkt. Magufuli amewataka wananchi wanaozunguka mradi huo kuutunza na kuhakikisha hawaharibu vyanzo vya maji katika eneo hilo la ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kuacha uvuvi haramu ambao umekuwa na madhara makubwa kwa wananchi.

Aidha, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Vyombo vya Dola kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaochafua vyanzo vya maji katika eneo la Ziwa Victoria.

Katika hafla hiyo ya Uzinduzi wa mradi wa maji Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA HamisiHussein Maarufu TABASAM, ameamua kuachana na chama chake na kujiunga na CCCM.

Mhe. Rais Dkt. Magufuli ameendelea kusisitiza msimamo wa Serikali kuwa hakuna mwanafunzi atakayepata ujauzito ataruhusiwa kuendelea na masomo na ameyataka Mashrika yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa yakipinga uamuzi huo kufungua Shule zao wenyewe ambazo zitawasomesha wanafunzi wanaopata ujauzito.

“Haiwezekani Serikali itoe pesa kuwasomesha wanafunzi halafu wapate mimba waendelee na masomo hilo haiwezekani, hizo NGOs zinazotetea hali hiyo zikitaka zijenge shule kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi watakaopata ujauzito”amesema Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amezungumzia uamuzi wa Serikali kupeleka Miswada Mitatu ya dharura Bungeni kuwa unatokana na umuhimu wa hilo katika kutetea maslahi mapana ya nchi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi.

Mhe. Rais Magufuli amewaonya wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Chama hicho kutojihusisha na rushwa kwa vile rushwa ni adui wa haki, hivyo, atakayebainika kutumia rushwa atapoteza sifa ya kuwa Mgombea.

Akizungunzia ujenzi wa barabara ya kutoka Kamanga hadi Sengerama kwa kiwango cha lami, Mhe. Rais Dkt. Magufuli amesema kwa sasa Serikali imeshampata mkandarasi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ili barabara hiyo ianze kujengwa katika kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Rais Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchni kufafanua kwa wananchi na kusimamia uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo zaidi ya 80 katika mazazo ya Kilimo, tozo 7 za Mifugo na tozo 5 za Uvuvi ambao lengo lake ni kuwaondolea kero wananchi.
Aidha, amesema Serikali inafanya uchambuzi ili kubaini wale wote waliotoa pembejeo hewa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha utoaji wa leseni mpya za uchimbaji na halikadhalika leseni ambazo zimeisha muda wake. Ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Geita ambao walizuia msafara wake katika maeneo mbalimbali wakati akiwa njiani kuelekea Chato.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Sengerema,Mwanza
04 Julai 2017

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.