Header Ads

Odinga Ampa Shavu Ali Kiba Amtumia Ndege Binafsi Kwenda Kenya

Odinga Ampa Shavu Ali Kiba Amtumia Ndege Binafsi Kwenda Kenya
Upepo mwanana bado unaendelea kumpuliza, staa namba moja wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ baada ya mgombea anayewakilisha Muungano wa Vyama vya Upinzani nchini Kenya (NASA), Raila Omolo Odinga, kudaiwa kumuita nchini humo. Kwa mujibu wa chanzo kisicho na chembe ya shaka, Kiba anayesumbua kwa sasa na wimbo wake wa Seduce Me, alipata mwaliko huo mwishoni mwa wiki iliyopita ikiwa ni saa chache mara baada ya Odinga kushinda kesi ya uchaguzi Katika Mahakama ya Juu aliyokuwa amemfungulia Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye mambo yalimuwia mazito.

Kenyatta alitangazwa mshindi wa nafasi ya urais na Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IBEC) katika uchaguzi uliofanyika nchini humo Agosti 8, mwaka huu ambapo Odinga alifungua kesi hiyo mahakamani. Baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote, iliufuta uchaguzi huo kwa kueleza kuwa tume ya uchaguzi haikuzingatia uadilifu.

ODINGA KICHEKO

Mara baada ya hukumu hiyo kutolewa mahakamani, Odinga alizungumza na wanahabari na kueleza hisia zake akisema alifurahishwa kwa kitendo cha mahakama hiyo kutenda haki hivyo kuwataka wapiga kura wake kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika baada ya siku 60 tangu hukumu hiyo itoke.

TUJIUNGE NA CHANZO

Kwa mujibu wa chanzo hicho makini kilicho karibu na Kiba, uongozi wa NASA ambao ulimtumia Kiba katika kampeni za uchaguzi wa awali, haraka ulimtumia mwaliko kwa ajili ya pati maalum ya kusherehekea hatua ya ushindi huo nchini Kenya.

“Yaani Kiba nyota inazidi kumuwakia. Baada tu ya Odinga ‘kumgaragaza’ Kenyatta kortini, wamemuita Kiba haraka sana ili aende kusherehekea nao ushindi huo. Si unajua tena alikuwa sehemu ya watu waliompigia kampeni Odinga katika uchaguzi uliopita?” Kilinyetisha chanzo hicho. Katika mazungumzo yake na Ijumaa Wikienda, chanzo hicho kilizidi kushusha ubuyu kuwa kutokana na umuhimu wa Kiba na kazi kubwa aliyoifanya wakati wa kampeni, NASA waliamua kumtumia Kiba ndege binafsi (private jet) ili awahi sherehe hiyo ya kukata na shoka na ikiwezekana wafanye mazungumzo ya ‘kuliamsha dude’ la shoo kampeni.

“Wamemtumia ndege fasta na hivi ninavyoongea na wewe, Kiba amesharuka na ndege, amesepa zake Kenya kwa ajili ya kuwahi ishu hiyo maalum. Wanaheshimu sana mchango wa Kiba hivyo hawakuwa tayari kumkosa,” kilisema chanzo hicho.

KENYATTA MAMBO MAZITO

Chanzo hicho kilizidi ‘kunyunyiza’ kwa kueleza kuwa, kutokana na jinsi Kiba anavyokubalika nchini Kenya na ukizingatia sasa hivi anakimbiza na Seduce Me, mambo yatakuwa mazito kwa mgombea wa Chama Tawala cha Jubilee, Kenyatta. “Wewe sasa hivi kila kona ni Wimbo wa Seduce Me. Umeshafikisha watazamaji zaidi ya milioni tatu tangu utoke na haujafikisha hata wiki mbili, atawashawishi sana Wakenya, sasa unategemea Kenyatta atakuwa na hali gani?” kilihoji chanzo hicho.

MENEJA WA KIBA AFUNGUKA

Ijumaa Wikienda lilimvutia waya mmoja wa mameneja wa Kiba, Aidan Seif ambaye alithibitisha mualiko huo wa Kiba, lakini hakutaka kuuzungumzia kiundani, zaidi ya kusema anawashukuru Watanzania kwa kuendelea kusapoti muziki mzuri.
“Ni kweli ameitwa Kenya lakini nisingependa kulizungumzia sana hilo kwa undani. Kikubwa niwashukuru Watanzania na niwaombe tuendelee kusapoti muziki mzuri kutoka kwa Kiba na wanamuziki wote wa RockStar4000,” alisema Aidan.
KIBA AENDELEA KUWEKA REKODI

Wakati hayo yakiendelea, Seduce Me ya Kiba imeendelea kuweka rekodi ya kutazamwa zaidi kwenye Mitandao ya YouTube, Vevo na itunes hivyo kushika namba moja kwa Afrika Mashariki.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.