Header Ads

Kipindupindu chapiga hodi Dodoma


MTU mmoja amefariki dunia na wengine nane kuugua ugonjwa wa kipindupindu mkoani Dodoma.

Watu hao wanasadikiwa kukumbwa na ugonjwa huo kwenye sherehe ya harusi iliyofanyika katika Kijiji cha Mlowa barabarani wilayani Chamwino.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Charles Kiologwe, alisema ugonjwa huo uliingia tangu Oktoba 19, mwaka huu.

Alitaja wilaya zilizokumbwa na ugonjwa huo ni Bahi, Chamwino na Kongwa.

 “Ni kweli ugonjwa wa kipindupindu umeingia katika mkoa wa Dodoma na kuna baadhi ya watu wameugua na mmoja amepoteza maisha kwa ugonjwa huo wilayani Bahi tangu ulipoingia katika mkoa wetu,” alisema Dk. Kiologwe.

Alisema ugonjwa huo uliibuka kwenye sherehe ya harusi ilikuwa katika Kijiji cha Mlowa Barabarani ambayo ilikuwa na mkusanyiko wa watu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Alisema baada ya sherehe hiyo kukamilika, kesho yake watu wawili wa familia hiyo waligundulika kuumwa ugonjwa huo.

Kufuatia hali hiyo, mganga huyo alisema timu ya madaktari wa mkoa kwa kushirikiana na wa wilaya ya Chamwino walifungua kambi ya muda ya ugonjwa huo.

“Baada ya kudhibiti ugonjwa huo kwenye Wilaya ya Chamwino walipata taarifa ya mgonjwa mwingine ambaye alikuwapo kwenye sherehe hiyo ambaye ni Mkazi wa Chibelela wilayani Bahi kuwa anaugua ugonjwa huo,” alisema.

Aliongeza: “Mume wa mgonjwa huyo wakati akimuuguza mke wake huyo hakujua kama ni ugonjwa wa kipindupindu kwa kuwa alikuwa akimuuguza kienyeji na matokeo yake na yeye akakumbwa na kipindupindu na kumsababishia kifo.”

Aidha alisema wagonjwa wengine wawili waliokuwa safarini wakitokea kijiji cha Mlowa barabarani waliugua ugonjwa huo na kulazimika kulazwa katika Kijiji cha Nkurabi ili kupatiwa matibabu.

“Pia wagonjwa wengine ambao wanasadikiwa walikuwa kwenye sherehe hiyo waligundulika kuugua kipindupindu na kulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Kongwa,” alisema.

Dk. Kiologwe alisema hadi sasa watu 9 wameugua ugonjwa huo na kati yao mmoja amefariki na tayari hatua zimechukuliwa kwa kufungua kambi za muda kijiji cha Mlowa barabarani (Chamwino), Chibelela (Bahi), Nkurabi (Manispaa ya Dodoma) na Kongwa.

Alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa kufanya usafi na kuzingatia kanuni zote za afya ili kujiepusha kukumbwa na ugonjwa huo.

“Pia kama mtu ataona mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa huo amkimbize kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili aweze kupatiwa matibabu,” alisema Dk. Kiologwe

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.