Header Ads

Steve Nyerere Atokwa Povu Kisa Wema Kukutana na Makonda

Steve Nyerere Atokwa Povu Kisa Wema Kukutana na Makonda


Siku tatu baada ya muigizaji maarufu wa filamu, Wema Sepetu kumuangukia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mchekeshaji nyota, Steve Mengere ‘Steve Nyerere’ amebwatuka vibaya kuhusiana na ishu hiyo.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa njia ya simu juzi akiwa njiani kurejea Dar es Salaam akitokea Dodoma, msanii huyo anayedhaniwa kufanikisha kwa kiwango kikubwa kurejea CCM kwa Wema Sepetu, alikiri wawili hao kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani, nyumbani kwa bosi huyo wa mkoa.

Wakiagana.
“Hakuna uadui wa kudumu katika haya maisha, isitoshe wale wote ni vijana, wamekutana wameombana msamaha na mambo yamebakia kuwa historia. Wanaangalia maisha mengine ya huko mbele kwa sababu safari bado ni ndefu,” alisema mchekeshaji huyo ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa kundi linalohamasisha uzalendo kwa watanzania.

Kuhusu kama kuna ahadi yoyote iliyo nyuma ya makubaliano baina ya wawili hao ambao kabla ya kutofautiana wanaripotiwa kuwa marafiki, Steve alisema hakuna kitu chochote zaidi ya wao kuamua kuachana na mambo ya zamani na kufungua ukurasa mpya.

“Hili ni funzo kubwa sana kwa wapambe, hasa wasanii, watu wakikorofishana wawe na akiba ya maneno, kuna watu walikuwa wanatoa maneno ya ovyo kwa mkuu wa mkoa kupitia kwa Wema, sasa leo hawa wamepatana, hivi sura zao wanazipeleka wapi?

“Haya mambo ya maisha, ukiona kuna jambo limewatokea watu, ni vizuri mtu ukawa na kiasi cha maneno, au wengine walikuwa wanamponda Wema kwa kupitia kwa mkubwa, sasa leo hii wanajisikiaje?” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kutoonekana kwa mama mzazi wa msanii huyo, Miriam Sepetu nyumbani kwake Sinza Mori, ikidaiwa kuwa huenda amefichwa sehemu kwa malengo maalum, Steve Nyerere alisema kada huyo wa Chadema yupo nyumbani kwake.

“Nani amekuambia mama hayupo? Yupo palepale nyumbani kwake na mambo yanaenda vizuri tu, wala watu hawana haja ya kumtafuta popote,” alisema Steve, akipinga habari za kutokuwepo nyumbani hapo kwa siku kadhaa sasa, ambako kumeripotiwa na magazeti ya Global Publishers.

Uhusiano wa Makonda na Wema uliingia dosari baada ya mkuu huyo wa mkoa kumtaja katika orodha ya kwanza ya watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya, Februari mwaka huu.
STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko
Chanzo: Global Publishers

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.