Header Ads

Mtoto Abakwa na Kuuawa Kikatili na Dereva ‘Boda Boda’

Mtoto Abakwa na Kuuawa Kikatili na Dereva ‘Boda Boda’


Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 ambaye pia ni mwanafunzi ameuawa kikatili baada ya kubakwa na muendesha pikipiki akiwa anaenda shule.Imeelezwa kuwa Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14 alikuwa anasoma darasa la sita katika shule ya Msingi ya Vikonge iliyopo wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na majeraha ya kisu ubavuni mwake na sehemu zake za siri kunyofolewa .

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Damas Nyanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi Jumanne tarehe 23 Januari 2018 saa moja asubuhi umbali wa kilometa moja na nusu kutoka shuleni kwake.

“Asubuhi hiyo ya tukio, marehemu akiwa ameongozana na mdogo wake wa kiume huku wakielekea shuleni walikutana na mwendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’ ambaye alikuwa hawamfahamu na kuwaambia kwamba atawapa lifti. Marehemu alipopanda mwendesha bodaboda alimzuia mdogo wake wa kiume asipande ambapo aliondoka akiendesha pikipiki hiyo kwa kasi isiyo ya kawaida huku kaka wa marehemu akiikimbilia bila mafaniko.“amesema Kamanda Nyanda.

Kamanda Nyanda amesema kuwa mdogo wa marehemu alitembea kwa miguu kuelekea shuleni baada ya kuchoka kuifukuza pikipiki hiyo, ghafla aliiona pikipiki ile iliyombeba dada yake ikiwa imeegeshwa karibu na kichaka kando ya barabara inayoelekea shuleni kwao na akaipita.

“Kaka wa marehemu bila shaka kutokana na umri wake kuwa bado mdogo baada ya kufika shuleni hakushughulika kumtafuta dada yake, aliingia darasani na kuendelea na masomo kama kawaida na baada ya muda wa masomo yaani saa nane na nusu alianza safari ya kurejea nyumbani bila kumtafuta dada yake,” ameeleza Kamanda Nyanda.

Hata hivyo, baada ya mtoto huyo kufika nyumbani wazazi wake walishtuka kumuona akiwa pekee yake ndipo walipomuhoji alikomuacha dada yake ndipo alipowasimulia kila kitu.

“Wazazi wa marehemu baada ya kupata maelezo hayo walipatwa na mashaka hivyo walimtaka mdogo wa marehemu awapeleke kwenye eneo alipoina pikipiki iliyombeba dada yake ikiwa imepakiwa karibu na kichaka. Mtoto huyo aliwaongoza wazazi wake ambao walikuwa wamefutana na majirani zao hadi kwenye eneo la tukio, walishtuka kuona kuwa kuna nyasi zilikuwa zimelala ndipo walipoona mwili wa marehemu ukiwa umechomwa kisu ubavuni huku sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa,“amesema Kamanda Nyanda.

Hili sio tukio la kwanza kutokea wilayani humo ambapo mwaka jana mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kipanga, Wilayani Tanganyika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 13 alikutwa amebakwa hadi kufa na mwili wake kutelekezwa vichakani.

Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na msako mkali kuwabaini wahusika wa tukio hilo ili kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.