Header Ads

AFARIKI DUNIA AKIVUA SAMAKI

Leonard Emmanuel (35) mkazi wa kijiji cha Luhama mkoani Mwanza amefariki dunia baada ya kuzama katika ziwa Victoria wakati akivua samaki.


Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Julai 13, 2018 katika kijiji hicho kilichopo Kata ya Bangwe Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema, ikielezwa kuwa marehemu alikuwa akivua samaki kwa kutumia ndoano huku akiwa katika maboya, badala ya mtumbwi.


Ofisa mtendaji wa Kata ya Bangwe, Benard Bwaila amesema baada ya kupata taarifa alifika eneo la tukio na kuanza kumtafuta marehemu na kukuta mwili wake ukielea.


Kufuatia tukio hilo, Bwaila amepiga marufuku watu kutumia vyombo vya uvuvi visivyo rasmi kwa maelezo kuwa wanahatarisha maisha yao.


Baba mkubwa wa marehemu, Yohana Masome ameieleza MCL Digital kuwa Emmanuel alikuwa na wenzake wakivua samaki lakini baada ya kuona upepo umekuwa mkali, waliamua kuondoka lakini marehemu alibaki na kuwaeleza kuwa anatafuta kitoweo cha watoto wake.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema hana taarifa za tukio hilo, kubainisha kuwa atatoa ufafanuzi atakapopata taarifa.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.