Header Ads

"Serikali inatarajia kufanya marekebisho ya sheria ya kudhibiti biashara ya usafirishaji wa binadamu'' Fella

Katibu wa sekretarieti ya kupambana na usafirishaji wa binadamu, Seperatus Fella. kesho ikiungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya kupinga usafirishaji binadamu, wadau kutoka serikalini na taasisi binafsi wamekutana kujadili namna ya kufanya udhibiti.
Mkutano umefanyika leo Julai 29, 2018 ukiangazia hali halisi ya biashara ya usafirishaji binadamu Tanzania, changamoto za kisera na kisheria zilizopo na namna ya kuzitatua.
Katibu wa sekretarieti ya kupambana na usafirishaji wa binadamu, Seperatus Fella amesema, "Julai 30 ya kila mwaka ni siku ya kupinga biashara ya usafirishaji binadamu. Tumeona ni vyema kukutana kitaifa kujadili mambo kadhaa kuhusu janga hili.”
Amesema upungufu katika sheria zilizopo ni miongoni mwa mada zilizochukua nafasi katika mkutano huo, wadau wakisema udhaifu huo unapunguza weledi na juhudi zilizopo.
"Serikali inatarajia kufanya marekebisho ya sheria ya kudhibiti biashara ya usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2008 ili kuiongezea makali," amesema Fella.
Mratibu wa mradi wa kupinga biashara ya kusafirisha binadamu unaosimamiwa na shirika la kimataifa la RTI, Edwin Mugambila amesema sheria iliyopo ina upungufu na hasa katika vipengele kuhusu njia za usafirishaji wa binadamu na hukumu kwa wanaojaribu kusafirisha binadamu lakini wakashindwa.
Amesema pia sheria haitoi maelekezo kuhusu hatima ya walioathiriwa na usafirishaji wa binadamu.
"Sheria bado haikidhi vigezo vya kukomesha biashara hii hatari, tunahitaji mabadiliko," amesema.
Amesema adhabu zinazotolewa kwa wanaokamatwa bado haitoshi kukomesha biashara hiyo.
Mugambila amesema sheria hutoa hukumu ya kifungo cha hadi miaka 10 jela au faini ya Sh150 milioni.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.