Header Ads

VIONGOZI WANAWAKE WAPEWA SOMO UTOAJI TAARIFA

Kamishna wa Maadili  Mhe. Harold Nsekela, kutoka Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa semina kwa Madiwani na wakuu wa idara wanawake kutoka Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Madiwani na wakuu wa idara wanawake kutoka Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika semina leo jijini Dar es Salaam.
Madiwani na wakuu wa idara wanawake kutoka Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na Kamishna wa Maadili  Mhe. Harold Nsekela.

Madiwani na wakuu wa idara wanawake kutoka Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kuwa na ujasili wa kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa maadili ya uongozi.

Akizungumza katika ufunguzi wa semina ya maadili kwa viongozi wanawake, Kamishna wa Maadili  Mhe. Harold Nsekela, kutoka Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, amesema kuwa ni asilimia moja ya wanawake ndio wanaoshiriki katika kutoa taarifa ya ukiukwaji wa maadili.


Amesema kuwa kutokana utafiti uliofanywa na vikundi mbalimbali uliokuwa unapima ushiriki  wa utoaji wa taarifa umeonyesha wanawake kuwa na mwamko mdogo wa kutoa taarifa juu ya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi wa umma.

Mhe. Nsekele amesema kuwa kutokana na hali hiyo, semina inaweza kuleta mabadiliko kwa kuwajengea uelewa viongozi wanawake katika mamlaka za serikali za mitaa kuhusu maadili ya viongozi wa umma.

"Baada ya kupata mafunzo wataweza kuwahamasisha na kuwaelimisha wanawake wezao katika ngazi ya kata na mitaa" amesema Mhe. Nsekela.

Ameeleza kuwa semina itawasaidia kuwa ujasiri kwa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika wanapokumbana na ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya viongozi wa umma.

Hata hivyo amefafanua kuwa majukumu ya msingi ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma ni pamoja na kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa maadili, kupokea na kuhakiki matamko ya mali na madeni ya viongozi wa umma.

Majukumu mengine ni kufanya uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa maadili pamoja na kutekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu kwa ajili ya kukidhi dhima ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa.

Hata hivyo washiriki wa semina hiyo wamesema kuwa elimu waliopata watakwenda kuwafundisha wanawake wengine katika jamii ili kuhakikisha inabadilika na maadili mema.

 Diwani wa Viti Maalum Kata ya Buyuni Chanika Hajjat Safina, amesema kuwa semina hiyo imewasaidia katika kuhakikisha wanakwenda kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

"Wanawake wengine wamekuwa hawajitokezi katika kufanikisha masuala mbalimbali ya kimaendeleo kutokana baadhi yao wamekuwa na hofu" amesema Safina.

Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kinondoni Barima Omary, ameeleza kuwa elimu ya maadili kwa viongozi wa umma inapaswa kuendelea kutolewa katika ili baadhi ya viongozi wabadilike.

Amesema kuwa kwa sasa kuna ukosefu wa maadili kwa kiwango kikubwa katika jamii, huku akisisitiza kuwa familia zinapaswa kuwajenga watoto katika maadili mema ili baadaye waje kuwa viongozi wazuri katika taifa la Tanzania.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.