Header Ads

Kuwachuja makada wanaorudi


Aliyekuwa mbunge wa Liwale, Zubery Kuchauka akitangaza uamuzi wake wa kuhama chama cha CUF na kurejea CCM katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ofisi Ndogo za CCM, jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally. Picha na Ericky Boniphace 

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaanza kuwachuja wanasiasa wa upinzani wanaojiunga nacho ili kuhakikisha hawana uchafu na hasa tuhuma za rushwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari akimpokea aliyekuwa mbunge wa Liwale (CUF), Zubery Kuchauka aliyeomba kujiunga na chama hicho.
“Tunawaamini sana na tunawataka sana waliobaki, lakini tutawachuja... Tumekuwa tuna namna ya kutokuaminiana katika siasa, tunataka kujenga tabia ya kuaminiana. Yeyote yule wewe nitajie, ukithibitisha kwamba ana nuka rushwa na tukampokea, uje uniulize.”
Mpaka sasa wabunge watano wa CUF na Chadema wamehamia CCM. Mbali na Kuchauka, mwingine kutoka CUF ni Maulid Mtulia (Kinondoni) aliyehamia mwanzoni mwa mwaka huu.
Wengine ni Mwita Waitara aliyekuwa mbunge wa Ukonga; Dk Godwin Mollel (Siha) na Julius Kalanga (Monduli) wote wakitokea Chadema.
CCM imepoteza mbunge mmoja, Lazaro Nyalandu aliyekuwa Singida Kaskazini aliyehamia Chadema.
Mbali ya wabunge, vyama vya upinzani vimepoteza madiwani wapatao 70 waliotimkia CCM. Pia, upinzani umepoteza wanachama na viongozi akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, jana, Dk Bashiru alisema CCM haiwezi kupokea wala rushwa na itawachuja wengine wanaotaka kuhamia chama hicho.
“Hatuwezi kumpokea mla rushwa, na sisi tumejiridhisha kuwa huyu (Kuchauka) si mla rushwa. Atakayejitokeza akasema huyu ni mla rushwa kwa ushahidi, atatimka,” alisema Dk Bashiru.
Sifa za kuhamia CCM
Akitaja sifa za kuhamia chama hicho, Dk Bashiru alisema ni pamoja na kuwa na uraia wa Tanzania.
“Hatuwezi kumpokea mgeni, kama si raia. Hatuwezi kumpokea mtoto kwenye siasa, huyu ni bwana mdogo? Hatuwezi kumpokea mtu ambaye hana sifa ya kuwa mwanasiasa kwa sababu za kisheria, huyu ana wendawazimu?” alisema.
Hata hivyo, alisema ni lazima kujenga tabia ya kuaminiana kwa kuwa wanaohamia pia wametoka kwenye vyama vya siasa vinavyotambulika kisheria.
“Huyu amekuja kwenye chombo cha CCM kinachoendesha siasa kwa Watanzania. Ametoka CUF chombo halali kinachowatumikia Watanzania. Kuna shida gani?” alihoji.
Kauli ya Kuchauka
Akieleza sababu za kurejea CCM, Kuchauka ambaye anarejea katika chama baada ya kujitoa mwaka 2005, alisema ameamua kurudi kwa kuwa kimerejea kwenye misingi ya Tanu.
Pia aliitaja migogoro ndani ya CUF kuwa imechangia kufikia uamuzi wa kuondoka chama hicho.
“Nilikuwa CUF lakini unaulizwa CUF gani? Sasa nimeamua kuacha migogoro. Kwa kuwa mbunge nina majukumu mengi. Kwa mfano, kulikuwa na uchaguzi, ukisimama kwenye jukwaa la chama upande wa (Profesa Ibrahim) Lipumba huruhusiwi, unatakiwa ukae jukwaa la Chadema, wakati hakuna bendera ya chama. Ndiyo maana nimeamua kurudi CCM ili kuondoka kwenye wasiwasi,” alisema.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni utekelezaji wa ahadi za uchaguzi za CCM akieleza ni ujenzi wa hospitali, shule na kupelekewa watumishi wa afya 80.
Kuchauka alisema licha ya kuwa mbunge wa upinzani, alitembelewa na mawaziri sita jimboni, hivyo ameona aingie CCM ili kupata ushirikiano zaidi.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.