Header Ads

Makamba afunguka Mtatiro kuhamia CCM
Dar es Salaam. Katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba amesema wanaoshangaa au kuhoji hatua ya aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CUF, Julius Mtatiro kuhamia chama hicho tawala wanapaswa kujiuliza kama walishangaa pia wakati mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye walipohamia upinzani.
Mtatiro juzi alitangaza kuachana na CUF na kuanza mchakato wa kujiunga na CCM.
Makamba aliyekuwa katibu mkuu wa CCM wakati wa utawala wa awamu ya nne, alisema mwanasiasa kuhama chama ni utashi wake na haipaswi kutazamwa kama jambo baya.
Alisema wanaohoji wapinzani wenye ushawishi kuondoka kwenye vyama vyao watambue pia CCM iliwahi kuwa na vigogo waliokwenda upinzani.
“Kuna mtu mzito kama Lowassa? Nakuuliza kuna mtu mzito kama Sumaye?” alihoji mwanasiasa huyo alipozungumza na Mwananchi kuhusu wimbi la wapinzani kuvihama vyama vyao.
Lowassa na Sumaye walijiondoa CCM na kujiunga Chadema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Makamba alisema kama ilivyokuwa kwa Lowassa na Sumaye walipoondoka CCM na kwenda upinzani vivyo hivyo kwa wapinzani kwenda chama hicho tawala.
Alisema kitendo kinachofanywa na wapinzani si kipya kwa kuwa kimewahi pia kufanywa na wanasiasa wengine.
“Mbona (Augustine) Mrema alihama CCM na kwenda kujiunga na NCCR- Mageuzi. Mbona Zuberi Mtemvu aliondoka CCM na kwenda kuanzisha chama chake cha upinzani. Kuhama chama ni hiari ya mtu wala sio ubaya,” alisema.
Makamba alisema wanaohama chama wanavutiwa na vyama wanavyohamia. Alisema hali inayoendelea sasa inaonyesha wanasiasa hao wanavyovutiwa na sera za CCM.
CUF walonga
Uongozi wa CUF upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba umejitokeza kujibu hoja zilizotolewa na Mtatiro ikiwamo mgogoro unaokikabili chama hicho.
Mtatiro akitangaza kujiondoa CUF, alitoa sababu kadhaa, ikiwamo kutaka kufanya siasa za maendeleo kwenye jukwaa sahihi na kuangalia mustakabali wake kisiasa.
Chama hicho kiliingia kwenye mgogoro mwaka 2016 wakati wa mkutano mkuu ulioongozwa na Mtatiro kwa lengo la kujadili barua ya kujiuzulu uenyekiti Profesa Lipumba mwaka 2015.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Abdul Kambaya akizungumza na waandishi wa habari jana alidai Mtatiro amechangia kwa zaidi ya asilimia 70 katika mgogoro ndani ya chama hicho.
Kambaya alidai Mtatiro akiwa mwenyekiti wa mkutano mkuu, alisababisha chama hicho kugawanyika kwa kutosikiliza maoni ya wajumbe na kuamua kuuendesha kibabe ili kulinda masilahi ya upande mmoja.
“Hakuna kitu ambacho Mtatiro amekifanya kwenye chama hiki, kubwa zaidi amesababisha migogoro, ana asilimia 70 kwenye migogoro ya CUF, hamna kitu kingine,” alidai Kambaya.
Alidai Mtatiro akiwa naibu katibu mkuu alikiingiza chama hicho kwenye mgogoro kutokana na ubadhirifu wa Sh300 milioni kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga.
Kambaya akizungumzia kauli ya Mtatiro kwamba aliasisi ilani ya CUF iliyolenga kutoa elimu bure, alisema si kweli kwa sababu suala hilo lilianza kuzungumzwa kuanzia mwaka 2000 kabla hata hajawa mwanachama.
Alisema mafanikio ya CUF yametokana na jitihada za muda mrefu hasa kwenye mikoa ya Kusini ambako walishinda majimbo saba.
“Wanasiasa walio-strong huwa hawakimbii migogoro ndani ya vyama vyao, bali wanakaa humohumo mpaka migogoro itakapokwisha,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha na kuwa chanzo cha migogoro, Mtatiro hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema alishazungumza kujitoa katika chama hicho alipozungumza na waandishi wa habari.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.