Header Ads

Simba kufungua pazia ligi kuu Bara

Claytous Chama raia wa Zambia
WAKATI leo Jumatano Simba ikianza kufungua pazia la Ligi Kuu Bara kwa kucheza na Tanzania Prisons, kikosi hicho kitamkosa kiungo wake fundi Claytous Chama raia wa Zambia, kutokana na kuendelea kukosa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ambayo imechelewa kutoka kwa timu yake ya zamani ya Power Dynamos ya Zambia na hivyo TFF kuwaambia Simba wasimtumie.

Hii itakua mechi ya pili ya kimashindano ambayo kiungo huyo ataikosa kutokana na kukosa ITC baada ya wikiendi iliyopita kuwa nje kwenye pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa.

Chanzo kutoka ndani ya Simba kimelidokeza Championi Jumatano kuwa kiungo huyo sambamba na mlinda mlango wao, Deogratius Munishi ‘Dida’, hawatakuwa sehemu ya mchezo kutokana na kukosa vibali vya kucheza, jambo ambalo limechangiwa zaidi na masuala ya kimtandao ambapo usajili wote umekuwa ukifanywa huko.

Claytous Chama
“Ishu ya Chama bado mambo ni magumu kwa sababu hadi leo (juzi) hatukuwa tumepata lolote juu ya kibali hicho na kusababisha kocha kumuondoa kwenye hesabu za watakaocheza dhidi ya Prisons.

“Suala lake limekuwa na mkwamo kwa sababu ya masuala ya kimtandao ambapo kila kitu kuhusiana na usajili kwa sasa kinafanywa huko, hivyo ndiyo maana mpaka sasa hakujapatikana nafasi ya yeye kupata kibali lakini sio yeye tu, hata golikipa wetu Dida naye bado hajapata kibali kitakachomruhusu kucheza mechi hii,” kilisema chanzo hicho.

Championi lilimtafuta Mratibu wa Simba, Abbas Ally ambapo alisema: “ITC zao bado hazijaja lakini tunaendelea kufuatilia, hilo ni suala la ‘system’, ndiyo maana unaona hadi sasa hawajapata, tunaendelea kufuatilia kwa karibu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).”

Pia Championi Jumatano lilimuuliza Chama juu ya hali hiyo ambapo alisema: “Hakuna tatizo la kukaa nje, kama hunioni kwenye mechi jua kila kitu kinafuatiliwa na uongozi.”

Msemaji wa Simba, Haji Manara, amesema jana kuwa Fifa wamewaandikia barua Chama cha Soka cha Zambia kuhakikisha kuwa hadi kufikia leo Jumatano ITC ya Chama iwe imefika.
“Wamesema kama haitakuwa hivyo, watashughulika nao,”

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.