Header Ads

AICT yakataa kuzungumzia kifo cha mwanakwaya


 
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la AICT, Elisha Isebuka amesema wameacha suala la mauaji ya mwimbaji wa kwaya ya vijana, Mariam Charles (pichani) mikononi mwa polisi.
Alisema polisi ndiyo wenye mamlaka ya uchunguzi wa tukio hilo na kwamba, jukumu la kanisa ni kuendelea kumshukuru Mungu kwa namna mtuhumiwa wa mauaji hayo alivyokamatwa.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na polisi juzi wakati akijiandaa kuingia katika nyumba ya kulala wageni ya Kisuma iliyopo maeneo ya Sokota-Chang’ombe, baada ya kufika hapo na kuchukua chumba.
Wakati mtuhumiwa huyo akikamatwa na polisi gesti, upande wa pili kama mwendo wa dakika moja lilipo kanisa la AICT, ibada ya kumuaga Mariam ilikuwa ikiendelea.
Mwili wa Mariam umezikwa juzi kwenye makaburi ya Maduka Mawili-Chang’ombe.
Jana, Mchungaji Isebuka aliwaambia waumini wa kanisa hilo kwenye ibada ya Jumapili kuwa amekuwa akipigiwa simu nyingi kutoka kwa watu wanaotaka kujua habari za tukio hilo, lakini jambo analoweza kusema ni kwamba polisi ndiyo wanaolishughulikia.
Aliwapa matumaini waumini wa kanisa hilo kuendelea kumtegemea Mungu akisema ndiye mwenye uwezo na kutaja mazingira ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kwani ni sehemu ya miujiza yake.
“Tuendelee kumtegemea yeye (Mungu) na nashukuru mtuhumiwa amekamatwa na ukiangalia mazingira ya kukamatwa kwake ni miujiza ya Mungu,” alisema.
Mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa alipelekwa Hospitali ya Rufaa Temeke kutokana na kuelezwa kuwa, alikuwa amekunywa vidonge kumi vya aina ya valium na konyagi ili afe kama Mariam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema juzi kuwa walimpeleka hospitali ya Temeke mtuhumiwa huyo baada ya kuwaambia kuwa amekunywa vidonge kumi vya valium ili afe kama Mariam.
Lukula alisema mtuhumiwa huyo ni mtaalamu wa maabara na mkazi wa Kilakala Temeke na kwamba, alikutwa na daftari aliloandika kujutia kumuua marehemu kwa wivu wa mapenzi.
Akizungumzia maendeleo ya afya yake, Lukula alisema anaendelea vizuri na yupo chini ya jeshi hilo.
“Alitibiwa na bado yuko mahabusu polisi,” alisema.
Frank anatuhumiwa kumuua Mariam katika kile kilichoelezwa ni wivu wa mapenzi.
Mwili wa Mariam (26), ulikutwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya East London iliyopo eneo la Buza anakodaiwa alikuwa na mchumba wake siku ya Jumatano wiki iliyopita.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.