Header Ads

Magufuli aeleza ugumu alioupata kumteua Mtaka


Rais John Magufuli amesema wakati wa mchakato wa kuwateua wakuu wa mikoa na wilaya, wasaidizi wake walimshauri kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka hafai kupewa nafasi yoyote hata ukuu wa wilaya.
Rais Magufuli amesema baada ya muda mfupi wasaidizi hao wameukubali utendaji kazi wa Mtaka. Mkuu huyo wa mkoa aliteuliwa mwaka 2016.
Akizungumza na wakazi wa Simiyu katika mwendelezo wa ziara yake Kanda ya Ziwa jana, Rais Magufuli alisema huenda baadhi ya viongozi wanaobezwa kuwa hawafai ndiyo wanaweza na ni jukumu la kila mteule wake kusimamia maendeleo.
Rais Magufuli alitumia muda mwingi kusifu hatua ambazo mkoa huo umepiga ikiwamo kuendeleza sekta ya viwanda pamoja na maendeleo ya ujenzi wa nyumba kwa wakazi.
“Mheshimiwa Mtaka umejitahidi na wilaya zako zote, umeijenga upya Simiyu lakini saa zingine wazuri huwa wanapigwa vita sana,” alisema Rais.
“Wakati najaribu kutafuta wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, Mtaka walisema hafai hata u-DC katika ripoti niliyopewa, naitoa hiyo siri hapa, hafai hata u-DC ndiyo recommendation niliyoletewa na vyombo vyangu.”
Mtaka aliteuliwa Machi 13, 2016 ikiwa ni miongoni mwa wakuu wa mikoa 26 walioteuliwa na Rais Magufuli miezi mitano tangu kupita kwa Uchaguzi Mkuu 2015.
Rais Magufuli alisema baada ya kutafakari mapendekezo hayo hakukubaliana nayo na kuamua kumteua kuongoza mkoa huo ambao kwa sasa umepiga hatua kubwa ya maendeleo.
“Nikasema Mtaka kweli hafai hata u-DC (ukuu wa wilaya), nikambandika nikampa u-RC (ukuu wa mkoa) niwakomeshe kabisa wale waliosema hafai.Nimeuliza tena hebu mniletee ripoti ya wakuu wa mikoa wanaofanya vizuri wakaleta Mtaka ndiyo namba one, namba mbili,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na umati wa watu.
Pia alisifu juhudi zinazofanywa na uongozi wa mkoa huo katika kuendeleza viwanda na kwamba mkuu huyo wa mkoa amekuwa mstari wa mbele kufuatilia utekelezaji wake kwa mawaziri huku akiahidi kuwaunga mkono.
Awali, Mtaka alipokuwa akitoa taarifa ya mkoa huo kwa Rais alisema kwa mwaka jana wamezalisha kilo milioni 70 za pamba na hadi kufikia mwezi huu wamezalisha kilo milioni 112 huku matarajio yakiwa ni kilo milioni 150.
Pia alisema kwa mwaka jana mkoa huo ulikumbwa na uhaba wa chakula ambapo Rais Magufuli aliagiza uongozi na mkoa kuongeza kasi ya uzalishaji ili kuwa na chakula cha ziada.
“Mwaka huu 2018 tumevuna ziada ya chakula, tuna ziada ya mpunga, mahindi, maharage na mazao yote jamii ya kunde,” alisema Mtaka.
Mradi wa barabara
Akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa barabara yenye urefu wa kilomita 49.7 kutoka Bariadi hadi Maswa, mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale alisema ujenzi huo ambao ulianza Julai utakamilika Julai, 2019.
Alisema mradi huo ni awamu ya tatu ya ujenzi wa kilomita 171.8 kutoka Bariadi hadi Lamadi na Mwigumbi hadi Maswa moja pamoja na wa madaraja mawili makubwa unaogharimu Sh237 bilioni ikiwa ni fedha za ndani.
Maagizo kwa halmashauri
Rais Magufuli aliwaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini kutenga asilimia 10 ya mapato kwa vikundi vya vijana (asilimia nne), wanawake (asilimia nne) na walemavu (asilimia mbili).
Rais alisema halmashauri nyingi hazitekelezi agizo hilo na kwamba viongozi hao wanatakiwa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa ili kuwasaidia kufanya shughuli za kiuchumi.
“Wabunge kwenye maeneo yenu simamieni hivi vikundi vitakavyopata fedha hizi, madiwani simamieni hivi vikundi ili uhakikishe kuna vikundi vya akinamama, wazee na vijana hili ni takwa la sheria ya bajeti,”alisema.
Ujenzi Hospitali
Rais Magufuli alimwagiza waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuwaweka ndani maofisa uvuvi watakaoshindwa kushughulikia uvuvi haramu kwenye maeneo yao huku akiwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kupambana na vitendo hivyo.
Awali, Rais alianza kwa kueleza namna Serikali ilivyodhamiria kutatua shida za wananchi ikiwamo maji, barabara na umeme huku akisisitiza kuwa baadhi ya miradi imekuwa haikamiliki kwa wakati kutokana na watendaji wasiowajibika.
Alisema mikoa ya Kanda ya Ziwa ina rasilimali nyingi ikiwamo samaki, lakini kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu kumekuwapo na uhaba wa samaki.
“Maofisa uvuvi hawa ndio wameleta uvuvi haramu na mimi nikuombe waziri wa Mifugo na Uvuvi anza kushughulikia maofisa wako, ukikuta mahali kuna uvuvi haramu na kuna ofisa uvuvi washike hao weka ndani.”
Awali, Waziri Mpina alisema atahakikisha rasilimali za ndani zinatumika vizuri kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya maji. “Natamani muone tutakavyowasilisha bajeti yetu ya mwaka ujao, ni sekta ambazo zilikuwa zimedharaurika lakini katika Serikali ya Awamu ya Tano na mimi kama waziri tutaleta mapinduzi makubwa,” alisema.
Wadau watoa maoni
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumzia kauli ya Rais Magufuli kuhusu ushauri aliopewa wakati akimteua RC Mtaka walisema vigezo vyake na vile vya wasaidizi waliompelekea taarifa na orodha ya majina vilitofautina.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, alisema Rais ana aina ya vigezo vyake mwenyewe anavyovihitaji katika kupata watendaji, lakini katika mchakato huo alitofautiana na wasaidizi wake ambao walimuona Mtaka hafai.
“Utawala wa Rais Magufuli unamtaka yule ambaye anaonekana hafai. Inaelekea alimjua vyema Mtaka kuliko wasaidizi wake ndiyo maana aliamua kumteua kushika wadhifa huo,” alisema Profesa Mpangala.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema utendaji kazi bora wa mtu unategemea na kiongozi aliye juu yake kwa namna anavyomwezesha katika mambo mbalimbali ikiwamo rasilimali watu na miundombinu.
“Utendaji kazi wa mtu unakuwa mzuri kutokana na vigezo anavyowekewa na kiongozi wa juu yake. Katika selection (uteuzi), kuna siasa nyingi zinafanyika, kuna baadhi ya watu hawataki mtu fulani apewe cheo kwa sababu akipata atakwenda kuharibu masilahi yao,” alisema Salim.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.