Header Ads

MAHAKAMA MKOANI RUKWA YATENGUA UAMUZI WA CHADEMA Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Rukwa, imetengua uamuzi wa Chadema mkoa wa Rukwa, wa kumfuta uanachama na kumvua udiwani, Dickson Mwanandenje aliyekuwa diwani wa kata ya Majengo mjini Sumbawanga.
Diwani huyo alituhumiwa kuwa msaliti ndani ya Chadema, akidaiwa kupanda jukwaani Agosti 4 mwaka huu katika mkutano wa hadhara wa mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly na kumsifia mbunge huyo na chama chake (CCM).
Uamuzi huo, umetolewa leo Septemba 11 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Rozaria Mugisa  baada ya upande wa mlalamikaji ukiongozwa na Wakili wa kampuni ya Budodi Advocates Zonal Law Chambers, Mathias Budodi kuwasilisha hati ya dharura mahakamani hapo.

Pamoja na kutengua uamuzi huo, pia mahakama imeagiza bodi ya wadhamini ya Chadema, Mwenyekiti wa Wilaya, Katibu wa Mkoa na Mkurugenzi kutomzuia diwani huyo kuendelea kufanya kazi zake za udiwani ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara katika kata yake na kuhudhuria vikao vyote halali vya halmashauri kama Diwani.

Hati ilikuwa ikilenga mahakama hiyo kumrejeshea Diwani huyo nyadhifa zake zote kuendelea na Shughuli zake wakati wakisubiri kesi ya msingi kuanza kusikilizwa ambapo anapinga kuvuliwa uanachama na udiwani.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mugisa amesema baada ya kuridhishwa na hoja za mlalamikaji, alitengua uamuzi wa viongozi wa Chadema mkoa wa Rukwa, kupitia baraza la kuu la mkoa  lililotangaza kumvua diwani huyo nafasi zake.

 Amesema viongozi hao walifanya uamuzi huo bila kufuata katiba.

Alisema katiba ya Chadema ya mwaka 2016, inaelekeza kuwa chombo chenye mamlaka ya kumjadili Diwani ni kamati ya maadili ya kanda na kupeleka mapendekezo kamati kuu ambayo inaweza kufanya maamuzi  hayo.
 Kadhalika diwani huyo  ana nafasi ya kukata rufaa katika halmashauri kuu ya chama hicho.
Awali, Wakili Budodi alisema kuwa baada ya viongozi wa Chadema ngazi ya mkoa kufanya maamuzi ya kumvua uanachama na udiwani, Mwandenje walimwandikia barua MKurugenzi wa Halmashauri hiyo kumjulisha kuwa mwanandenje sio diwani tena ambapo nae alimjulisha Diwani huyo.
Wakili Budodi alisema walifungua kesi namba 5 ya mwaka 2018 na kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, walitoa notisi ya siku 30 kwa mkurugenzi huyo kutoendelea na mchakato wowote hadi kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa Septemba 20, mwaka huu.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.