Header Ads

Musukuma akiri kudaiwa


Baada ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kupitia kampuni ya udalali ya LJ International Ltd kutangaza kuzipiga mnada mali za mbunge wa Geita vijijini, Joseph Musukuma, mwenyewe ameibuka na kuzungumzia jambo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jana Ijumaa Septemba 7, 2018 jijini Mwanza,  Musukuma amekiri kudaiwa na benki hiyo na kubainisha kuwa hakuna mali yake hata moja itakayouzwa.
Mali za mbunge huyo zilizotajwa kupigwa mnada ni pamoja na kiwanja Na.275 Block kilichopo Mbezi Dar es Salaam na kiwanja Na. 2 block A kilichopo Korogwe mjini.
Mali nyingine ni shamba Na.201 lililopo kijiji cha Igate mkoani Geita, kiwanja Na.116 block A Buswelu Kaskazini na kiwanja Na.48 block T katikati ya jiji la Mwanza.
“Suala la mimi kukopa benki ni la kikatiba na lipo kisheria kwa kuwa mimi ni mfanyabiashara wa kati,” amesema.
“Kuhusu hili linalozunguka mtandaoni lisiwakatishe tamaa wapiga kura wangu, hakuna mali yoyote itakayouzwa.”
Mbunge huyo ametoa siku saba kwa mkurugenzi wa mawasiliano wa NBC, Wiliam Kalage kuthibitisha maneno aliyoyatoa kwa waandishi wa habari kuhusu mnada huo.
Amebainisha kuwa atakwenda mahakamani kuishtaki benki hiyo pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kwa kumchafua.
“Suala hili limeanza kuandikwa tangu 1999 nilipoanza kugombea ubunge, likaja kuandikwa tena 2003 na kampeni za mwaka 2015,” amesema.
“Hii ni mara ya nne limeandikwa nikiwa kwenye kampeni Monduli, lengo lao ni kutaka kuharibu sifa ya Msukuma.”
Licha ya  kukiri anadaiwa na benki hiyo, amesema analipa deni kidogo kidogo na hana tatizo na NBC.
“Suala la (NBC) kunipeleka kwenye vyombo vya habari halijanifurahisha,” amesema.
Mbali na Musukuma, kampuni ya LJ International Ltd pia imetangaza watu 19 wanaodaiwa na benki hiyo ambao mali zao zitanadiwa.
Soma Zaidi:


Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.