Header Ads

Waliogushi vyeti serikalini waagwa rasmiBaada ya zoezi la ukaguzi wa vyeti kwa wafanyakazi wa ngazi mbalimbali serikalini lililofanyika kuanzia mwaka 2016 na kubaini uwepo wa waliogushi na wasio na vyeti kabisa, hatimaye serikali imeziba nafasi za walioondolewa.

Serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Capt. (Msataafu) George Mkuchika, imetangaza kutoa kibali cha kuajiri cha watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililoachwa na watumishi hao walioondolewa kwenye utumishi.
Mkuchika amebainisha hilo leo bungeni Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Aida Khenani kuhusu mkakati wa Serikali wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti feki.
"Tayari nafasi hizo zimeshaanza kuzibwa maana serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi wapya katika ngazi ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waajiri wote wameendelea kujaza nafasi hizo," alisema Mhe. Mkuchika.
Mkuchika ameongeza kuwa Serikali imetoa vibali vya ajira kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa mara mbili ambapo cha kwanza kilitoka tarehe 22 Agosti, 2017 kikifuatiwa na cha Machi 12, 2018 kwaajili ya kuziba nafasi zote za Watendaji wa Vijiji na Mtaa zilizoachwa wazi.
Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutambua umuhimu wa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 22,150 wakiwemo watumishi wa kada za Ualimu 6,840, Fundi Sanifu wa Maabara za shule 160, kada za Afya 8,000, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu 624 na watumishi 6,526 wa kada nyingine.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.