Header Ads

Juhudi zinahitajika kuweza kumaliza tatizo la Afya nchini


Barani Afrika, unapozungumzia masuala ya afya, vipaumbele vinakuwa upatikanaji wa huduma hizo kwa njia za uhakika, uwepo wa hospitali bora (majengo na miundombinu), uwepo wa rasilimali watu za kutosha (madaktari, wauguzi, wataalamu na watoa huduma), usambazaji wa dawa wa uhakika, unafuu wa bei za dawa na upatikanaji wa vifaa muhimu hospitalini bila kusahau sera na sheria jumuishi ambazo zinatoa jukumu kwa serikali kuhakikisha hakuna mwananchi anakufa kwa kukosa matibabu.

Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi, upatikanaji wa huduma za afya umekuwa mgumu na kuna maelfu ya watu wanakosa matibabu ya uhakika, hospitali nyingi zilizopo hazikidhi mahitaji (hasa vijijini) na zilizoko mjini zina changamoto nyingi za kiutawala na kimfumo ambazo zinakwamisha huduma.

Kuna madaktari, wauguzi, wakunga, wataalamu na watendaji wa sekta ya afya wachache – kuna upungufu mkubwa kwenye eneo hili kiasi kwamba kuna madaktari kazi zinawazidia, hawalali kwa sababu wana zamu nyingi za kuhudumia wagonjwa kupita uwezo wa kibinadamu na juhudi za kuajiri madaktari wapya zimekuwa mtihani kwa sababu serikali haina bajeti ya kutosha.

Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kuongeza bajeti ya afya kutoka chini ya bilioni 50 kwa mwaka hadi zaidi ya bilioni 200, bado kumekuwa na changamoto tele ambazo kama hazitafanyiwa kazi, sekta ya afya nchini itaendelea kudorora.

Kwanza, lipo suala la ucheleweshwaji wa kupandisha hadhi vituo vya afya au zahanati ambazo zinatoa huduma muhimu vijijini na mijini umekuwa tatizo lisilo na tiba ya haraka ndani ya hii miaka miwili ya uongozi wa awamu ya tano. Zipo Zahanati kadhaa ambazo zimejiendeleza na kuwa na uwezo wa kuokoa maisha ya wananchi wengi vijijini na mijini, na vipo vituo vya afya ambavyo vimefikia hadhi muhimu ya kupandishwa hadhi lakini jambo hilo halifanyiki.

Baadhi ya wamiliki wa zahanati na vituo hivi vya afya wanasema kuwa wanahitaji tu zahanati na vituo hivyo vipandishwe hadhi na kisha Serikali isaidie daktari mmoja au wawili wa ziada na kuziacha zichape kazi kuokoa maisha ya maelfu ya wagonjwa. Kwa bahati mbaya hadi sasa Serikali imekuwa inashindwa kutoa msaada na ushirikiano kwa zahanati na vituo hivyo, jambo ambalo lina maana mbaya sana kwa mustakabali wa sekta ya afya nchini.

Sekta ya afya bado inafanya vibaya kwenye eneo la utoaji wa bima za afya. Kwa hakika hakuna juhudi kubwa zinazoonekana za kuhakikisha Watanzania wote wenye uwezo na wasio na uwezo wanaunganishwa kwenye bima za afya, hili ni tatizo kubwa kushinda linavyochukuliwa au linavyoelezwa na wizara.

Kwa hali ya dunia ya sasa, hatari zake na mazingira ya kiafya – ni vigumu kwa mtu binafsi kujitibu kwa fedha taslimu. Takwimu za wizara zinaonesha kuwa hadi mwaka huu 2017 wizara imeweza kuongeza wanachama wa bima ya afya kutoka 702,598 mwaka 2015/16 na kufikia wanachama takribani 800,000.

Hii ni nchi yenye raia zaidi ya milioni 55 hivi sasa, kama hadi leo ni Watanzania chini ya milioni moja ndio wamepata uwezo wa kukata bima ya afya ya taifa basi kuna shida inayohitaji utatuzi wa haraka. Na tena kama ukitazama kwa umakini unagundua hilo linafanyika kwa sababu serikali ina wafanyakazi takribani 500,000 na hivyo hao ndio wamepandisha idadi hiyo kirahisi.

Kwa maana hiyo huko mitaani kuna zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania ambao hawajajiunga kwenye hata Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya ambao tunategemea uwe kiashiria kikuu cha mafanikio ya sekta ya bima za afya kwa kulinganisha na bima zingine binafsi za afya.

Sekta yetu ya afya haijafanikiwa sana kupambana na magonjwa ya mlipuko, katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita magonjwa ya milipuko yamechukua maisha ya Watanzania ambao walikuwa msingi wa nguvu kazi ya uzalishaji wa taifa.

Ndiyo maana pia, Septemba 2017, shirika la Afya Duniani (WHO) liliitaja Tanzania kati ya nchi 10 duniani zenye watu wanaougua ugonjwa wa kipindupindu. Kwa hiyo hali ya mashambulio ya magonjwa ya milipuko ni jambo linalohitaji nguvu ya ziada ambapo lazima kuwe na ufuatiliaji, ukaguzi na uondoaji wa vyanzo vya magojwa haya.

Changamoto kibao za wizara
Inawezekana wizara inayoshughulika na afya ina mzigo mkubwa unaotokana na masuala mengine inayoshughulikia. Masuala yote ya jinsia, wanawake, watoto, wazee yanashughulikiwa na wizara ya afya.

Moja ya programu ambazo zimeanzishwa ni kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na takwimu zake zinaonyesha kuwa zaidi ya Sh170 Bilioni zimetolewa kwenda kwenye vikundi vya wanawake wajasiriamali katika baadhi ya halmashauri, Benki ya Wanawake Tanzania na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Udhaifu mkubwa na wazi ambao umekuwepo kwenye njia hizi za uwezeshaji wanawake ni kwamba sehemu kubwa ya wanawake ambao wamekuwa wakipata mikopo hii ni wale ambao wako karibu sana na CCM na hata njia za utolewaji mikopo hii siyo za wazi sana.

Hili ni tatizo ambalo lisipotatuliwa mikopo hii itakosa nguvu na umuhimu wake na hatimaye itakuwa inatumika kama njia ya kulipa fadhila kwa makundi fulani ya kijamii au ya wanawake badala ya kutatua tatizo la msingi kwa wanawake wote.

Rais John Magufuli alitoa msimamo wa kutowasomesha wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni.

Katika tamko hilo la Juni 22, 2017, alisema kuwa katika kipindi chake cha utawala, mwanafunzi yeyote wa kike (shule ya msingi na sekondari) akipata mimba ni marufuku kurudi shuleni. Na kwamba hawezi kufanya kazi ya kusomesha wazazi.

Hatua hii ilichukuliwa licha ya kuwapo mikakati tofauti na ya muda mrefu ya serikali juu ya watoto wa kike, hali halisi ya mtoto wa kike nchini Tanzania, sera juu ya mtoto wa kike na haki ya kulindana msichana.

Pia iliendana kinyume na matamko mbalimbali ya kisera yaliyowahi kutolewa katika miaka ya hivi karibuni na serikali yenyewe yaliyosisitiza kuwa wasichana wenye mimba watasaidiwa na Serikali kurudi kusoma.

Suala la kuwasaidia wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni ni la haki yao ya msingi, ni ulinzi wa taifa na vizazi vyetu ni suala la kisera na tena sera muhimu kwelikweli.

Asilimia 27 ya wasichana walioko shuleni wanaathirika na mimba za utotoni nchini Tanzania, vyanzo vikubwa vya mimba hizo ikiwa ni umaskini na mila potofu. Kama watoto wanaopata mimba hawatasomeshwa, wakati tafiti zinatuonyesha vyanzo vya mimba hizo ni umasikini wetu na mila zetu, haya yatakuwa makosa makubwa sana.

Hitimisho
Pamoja na matatizo yote tuliyonayo, Sera ya taifa letu ya kutoa matibabu bure kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 60 na watoto wa chini ya miaka mitano imebaki kuwa “mazingaombwe.”

Wazee wamesahaulika kwenye matibabu na hadi sasa hakuna mipango ya kweli na ya wazi ya Serikali kuwakwamua kutoka kwenye vifo vya mara kwa mara ambavyo vingeepukika.

Pamoja na kuwa Waziri Ummy Mwalimu akisaidia na Dk Ndungulile wanaonyesha uwezo mkubwa katika kuiongoza wizara hii, kazi iliyoko mbele ni kubwa mno kwa sababu uhalisia wa hali ya matibabu nchini kwetu ni tatizo kubwa na lenye kushtua

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.