Header Ads

Mwanamke akamatwa kwa tuhuma za kughushi risiti za kielektroniki (EFD)


DOREEN Urassa (40) mkazi wa Kunduchi, jijini Dar es Salaam amekamatwa kwa tuhuma za kughushi risiti za kielektroniki (EFD) za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Doreen na mwenzake Raymond Alexander (31) mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, walikamatwa wakifanya kitendo hicho juzi katika eneo la Sinza Mori, Mkurugenzi  Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema jana.

Oktoba 4, majira ya saa 1:00 jioni, tulifanikiwa kuwakamata watu wawili maeneo ya Sinza Mori wakiwa wanagushi risiti za EFD. Watuhumiwa hawa tutawafikisha mahakamani kwa hatua za kisheria", alisema Kayombo.

Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa watu wote wanaojishughulisha na mchezo huo  kuacha mara moja kwa kuwa TRA itaendelea kufanya msako mkali na mtu yeyote akibainika, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Kayombo aliwaomba wasamaria wema waendelee kutoa taarifa za kuwafichua wanaogushi risiti na kuwahakikishia kuwa majina yao hayatatajwa popote.

"Mamlaka haitamvumilia mtu yeyote anayejaribu kukwamisha ukusanyaji mapato ya serikali, iwe kwa kugushi risiti,  biashara ya magendo au njia nyingine yoyote ya udanganyifu. Tunawaomba wasamaria wema waendelee kutupa ushirikiano kwa kuwafichua watu wadanganyifu na tunawahakikishia kutunza siri kwa kutoyataja majina yao popote pale," alisema.

Kayombo alisisitiza kuwa TRA inaendelea kuwasaka watu wote wanaojishughulisha na vitendo vya kugushi risiti ikiwa ni pamoja na kukamata biashara za magendo.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.