Header Ads

Sababu ya kusitisha huduma kwa zahanati 9 na Hospitali zinazomilikiwa na marie stopes Tanzania zatajwa


Hali ya sintofahamu imetanda baada ya zahanati tisa na hospitali zinazomilikiwa na Marie Stopes Tanzania (MST), kusitisha utoaji wa huduma kwa muda wa wiki tatu sasa kutokana na kile kinachodaiwa kufanyiwa ukaguzi na Serikali.
Vituo hivyo vilivyopo Tanzania Bara katika maeneo ya Arusha; Mwanza; Musoma mkoani Mara; Iringa; Mbeya; Kahama mkoani Shinyanga; Temeke, Kimara, Mabibo na Hospitali ya Mwenge jijini hapa vimesitisha utoaji huduma isipokuwa kituo cha Zanzibar.
Msemaji wa Marie Stopes Tanzania, Dotto Mnyadi alisema wamesitisha upokeaji wa wagonjwa wapya katika vituo vyao kutokana na ukaguzi unaofanywa ikiwa ni jambo la kawaida kwa hospitali hizo kukaguliwa.
Mwananchi lilipomtafuta msemaji wa Wizara ya Afya, Catherine Sungura kujua lini ukaguzi huo utakamilika na iwapo kuna sababu nyingine zilizosababisha kusitishwa kwa huduma katika taasisi hiyo, alisema hana taarifa.
“Wizara haina taarifa ya kuvifungia vituo hivyo na msajili hajafanya zoezi hilo,” alisema Sungura.
Alipotafutwa naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayehusika na masuala ya afya, Josephat Kandege alisema taarifa rasmi kuhusu suala hilo kutoka serikalini zitatolewa kesho.
“Hili suala halijakamilika kwa maana Manispaa ya Kinondoni hawana taarifa kuhusu hilo, Wizara ya Afya hawana taarifa kilichoonekana ni bodi ya wamiliki wa vituo vya afya binafsi ndiyo waliopo nyuma ya hili,” alisema.
Wagonjwa walalamika
Kwa muda wa nusu saa ambao Mwananchi jana liliweka kambi katika Hospitali ya Marie Stopes Mwenge, baadhi ya wagonjwa waliofika walionekana kuingia na kutoka walipokosa huduma.
Daines Mbaga alisema, “Nilifuata huduma za mama na mtoto hapa, lakini nimeelekezwa kwamba niende Sinza Palestina huko nitapata.”
Baadhi ya wagonjwa walilalamikia usumbufu walioupata wakidai ingekuwa bora uongozi wa Marie Stopes wangetoa matangazo ya kusitisha huduma kuliko kukaa kimya hadi watu wanafika hospitali.
“Tungefahamishwa na kama kuna ukaguzi unaendelea hatuoni sababu ya kuzifungia kutoa huduma, wakumbuke ni Watanzania wengi tunategemea huduma za hizi hospitali,” alisema Amina Juma.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya watu wanaotegemea vituo hivyo kupata huduma, Mnyadi alisema wamekuwa wakiwaelekeza wagonjwa mahali ambako watapata huduma pindi wanapofika.
“Kwa mfano kwa wanaofika hospitali ya Mwenge hawa inategemea ana tatizo gani. Wapo tunaowaelekeza Umati, Trust Clinics na Sinza Palestina kwa kuwa pale kuna kitengo cha mama na mtoto, na kwa bahati wakienda huko serikalini huduma ni bure,” alisema. Hata hivyo alisema Serikali imekuwa ikivifanyia ukaguzi vituo hivyo mara kwa mara kwani wamekuwa wakitoa huduma za afya ya uzazi kwa wigo mpana.
“Marie Stopes tunachangia asilimia kama 30 ya huduma za afya za uzazi, wenzetu hawafanyi Tanzania nzima na hata kama wanafanya ni katika maeneo machache, kuna mashirika mengi yana hospitali ila ni moja - sisi tumezagaa nchi nzima.”
Alisema licha ya kutoa huduma katika vituo vyao, pia wanazitoa kupitia kliniki zinazotembea kwenye hospitali za umma hasa vijijini.
Mnyadi alipoulizwa kuhusu wiki tatu za kutotoa huduma na wafanyakazi waliopo iwapo watalipwa au vinginevyo alisema, “MST ina wafanyakazi 400, wafanyakazi wetu wanaendelea kuja kama kawaida kazini na kuna kazi ambazo zinaendelea kufanyika.”
Alipoulizwa kuhusu taarifa za madai ya hospitali hiyo kujihusisha na utoaji wa mimba, alisema hazina ukweli na kufafanua kuwa hawajawahi kuhusika na vitendo hivyo. “Hospitali inatoa huduma ya mimba baada ya kuharibika (CPAC), hii ipo kisheria na kwa mwongozo wa Wizara ya Afya japokuwa tunapokea idadi kubwa ya waliotoa mimba vichochoroni wanapofika hapa tunawahudumia ili kuokoa maisha yao,” alisema.
Kuhusu taarifa za kufungiwa kutokana na kujihusisha na uzazi wa mpango, alisema, “Hapa nchini ni mashirika mengi yanajihusisha na uzazi wa mpango, kama ndivyo basi hata Umati na wengineo wangefungiwa au mashirika yote yafungiwe kitu ambacho si kweli.”
Mwananchi lilitaka kujua ni lini huduma zitarejea? “Hatuwezi kusema ni lini zitarejea mpaka ukaguzi utakapomalizika na (wahusika) watakapoona nyaraka zao zote zimekamilika watatufungulia na tutaendelea kutoa huduma, lakini kwa kipindi hiki pia kuna ukarabati tunaendelea nao.”
Alisema Marie Stopes inaendelea kutoa huduma zake kama kawaida kwa kuunga mkono juhudi za Serikali.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.