Header Ads

Wabunge wapewa onyo kutotoa siri za ndani ya vikao
DODOMA:Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania,  Anne Makinda amewaasa wabunge kutotoa siri za ndani ya vikao vya Bunge kwani wanajidhalilisha kwa wapiga kura wao.

Makinda ametoa kauli hiyo  jana wakati akizungumzia masuala ya uongozi kwa Azaki katika ukumbi wa LAPF jijini hapa ambapo ametaja mambo mawili kama ndiyo siri ya Bunge kuwa, hairuhusiwi kuzungumza nje ya Bunge mambo wanayolumbana ndani wabunge lakini kuvumiliana ni jambo la msingi pia.

Kauli ya Makinda imekuja wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likituhumiwa kuwanyima Watanzania haki ya kupata taarifa kwa kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya runinga wakati mijadala ya bunge hilo likiendelea.

Spika huyo wa Bunge la kumi amesema baadhi ya watu wakipewa madaraka huwa wanajisahu na wakati mwingine kufikiria kuwa wamepewa nafasi ya kujinufaisha jambo alilosema linawaondolea sifa ya kuwa viongozi.

Amewashauri viongozi kujenga tabia ya kuvumiliana na kuchukuliana lakini akasisitiza suala la Amani kwamba itajengwa katika msingi huo lakini wakiyumbishana inaweza kuondoka na kuepelekea kuvurugana.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo amesema bado kuna tabia ya watu kutokujenga tabia ya kurithishana madaraka kama wanavyofanya maeneo mengine akitaja hofu na kutojiamini kwa baadhi ya walioko madarakani na ndiyo sababu wengine hata wanashindwa kuomba likizo wakihofia nafasi zao kutekwa na wengine.

Kuhusu wanawake amesema wasitake kubebwa zaidi bali wapambane katika nafasi mbalimbali ili wazipate akatolea mfano kuwa yeye alikuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa wagumu wa kukatishwa tamaa na hasa alipokuwa anagombea kwani alitukanwa hadi matusi ya nguoni lakini alisonga mbele tu.

Amesema alistaafu bungeni akiwa ametumikia miaka 40 lakini anachojivunia zaidi ni mchakato wa kutunga sheria ya bajeti ambayo alifanya kazi hiyo kwa kushauriwa na aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Otouh.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.