Header Ads

Chirwa amjibu Zahera, kukataliwa Yanga


Obrey Chirwa na Mwinyi Zahera

Baada ya kocha wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera kusema waziwazi kuwa haitaji kumsajili mchezaji, Obrey Chirwa katika kikosi chake, hatimaye Chirwa ameibuka na kumjibu kocha huyo.
Chirwa ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo kwa misimu miwili, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Azam Fc wiki hii baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Nogoom El Mostkabl FC ya Misri baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipa stahiki zake za kimkataba.
Tetesi za Yanga kumsajili Chirwa zilianza kusambaa mara baada ya mchezaji huyo kuonekana jukwaani katika moja ya mchezo wa Yanga katika uwanja wa taifa, ambapo tetesi hizo zilikufa baada ya kocha Zahera kusema kuwa hamuhitaji mchezaji huyo tena kwenye kikosi chake kutokana na tabia yake ya kugomea mazoezi, kugoma kucheza na hata kusafiri na timu pindi klabu inapokuwa na matatizo ya kiuchumi.
Akizungumza na wanahabari juu ya kukataliwa na kocha Zahera katika klabu ya Yanga, Chirwa amesema,
"Kwa hilo mimi siwezi kumchukia kocha, namtakia afanye kazi vizuri kwasababu yeye ni kama baba yangu, kwahiyo namtakia afanye vizuri wala sina ugomvi naye," amesema.
"Mimi popote pale naweza kufanya kazi, yeye ni kama mzazi wangu. Mwenyewe alishasema kuwa Chirwa simtaki kwakuwa anagoma, watu ndiyo wako hivyohivyo na mimi niko hivyo wala siwezi kubadilika, kila mtu ana msimamo wake. Kama kampuni haikupi kitu mlichokubaliana lazima utatafuta mahala pengine," ameongeza.
Pia Chirwa amesema kuwa anataka kuzifunga Simba na Yanga ili jina lake liendelee kuwa juu, pamoja na kuongezewa mkataba wake katika klabu yake ya Azam.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.