Header Ads

Dkt. Shein atoa neno kwa wakina mama kuhusu SarataniRais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka akinamama kote nchini kupeana elimu juu ya umuhimu wa kuchunguzwa saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kuwataka  watoto wa kike kuhudhuria vituo vya afya kupata chanjo ya maradhi hayo.

Amesema hatua hiyo itawezesha kugundulika mapema viashiria vya kuwepo maradhi hayo na hivyo kuweza kupata tiba sahihi na kwa wakati muafaka.

Dk.  Shein amesema hayo leo katika hafla ya  uzinduzi wa mradi wa uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi, iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil, Kikwajuni mjini hapa.

Mradi huo wa miaka minne unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Afya pamoja na Kamisheni ya Afya na uzazi wa mpango, kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China.

Dk. Shein alisema kuna umuhimu mkubwa kwa akinamama kuhimizana na kupeana elimu, ili kila mmoja aone umuhimu na faida ya kwenda kuchunguzwa maradhi hayo, sambamba na kuwahimiza watoto wa kike walio na umri kati ya miaka tisa hadi 14 kupata chanjo kama inavyoelekezwa na wataalamu.

Alisema katika kufanikisha jambo hilo, ni muhimu kwa akinababa kuiunga mkono jinsia hiyo ili kuepukana na athari mbali mbali zinazoweza kujitokeza, ikiwemo uchelewaji wa kupata matibabu.

Alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadhamini wa mpango huo watawahudumia na kuwapatia matibabu sahihi na kwa wakati muafaka wale wote watakaobainika kuwa na matatizo, hatua hiyo ikiwa ni kuzingatia sera ya Serikali ya kutowa matibabau bure kwa wananchi bila ya ubaguzi.

Dk. Shein alieleza kufarijika na kampeni  iliyofanywa na Serikali ya kuwapatia chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14, ambapo uzinduzi wake ulifanyika April, mwaka huu.


Akigusia ukubwa wa tatizo hilo, Dk. Shein alisema ugonjwa huo thakili umekuwa ukipoteza roho za watu wengi hapa nchini na kubainisha kuwa taasisi ya Saratani ya hospitali ya Ocean Road imeripoti kuwa jumla ya wanawake 35,000 hupata saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka, huku asilimia 20 pekee ndio hufika katika taasisi hiyo kwa matibabu.

Aidha, alisema takwimu za maradhi hayo katika Kilinik ya Hospitali ya Mnazimmoja inaonyesha kuwa asilimia 80 ya wanawake wenye aina hiyo ya saratani, hufika hospitali kwa ajili ya matibabu, wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.