Header Ads

JKT Tanzania wakoshwa na uteuzi wa Rais Magufuli


Klabu ya soka ya JKT Tanzania inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania Bara, imeeleza kufurahishwa na uteuzi wa Rais Magufuli ambaye jana Desemba 7, 2018 alimteua Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Akiongea na    www.eatv.tv  Msemaji wa JKT Tanzania, Jamila Mutabazi amesema uteuzi huo ni furaha kwao kutokana na namna ambavyo kiongozi huyo amesaidia michezo jeshini wakati wa uongozi wake.
''JKT Tanzania tumefurahishwa sana na uteuzi huu, imani yetu kuwa atafanya vyema kwenye majukumu yake kama ambavyo imekuwa kawaida yake. Tumekaa naye kwa muda mrefu kama kiongozi wetu na amekuwa na mchango mkubwa sana kwetu kama timu'', amesema.
Aidha Jamila amesisitiza kuwa mchango wa kiongozi huyo kwenye michezo jeshini hauwezi kusahaulika na ndio maana wao kama JKT Tanzania waliamua kumpa heshima ya jina la uwanja wao wa nyumbani kwa kuuita Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Uwanja huo upo maeneo ya Mbweni Dar es salaam.
Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Desemba 3, 2016 kabla ya kustaafu mwanzoni mwa mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na Meja Jenerali Martin Busungu.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.