Header Ads

Makambo na kocha wa Yanga wang'ara tuzo za TPL

Mshambuliaji wa klabu ya Yanga, Heritier Makambo amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.

Makambo raia wa Congo (DRC), alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Said Dilunga wa Ruvu Shooting na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wa Yanga alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mwezi huo wa Novemba, Yanga ilicheza michezo minne, ambapo Makambo alitoa mchango mkubwa kwa Yanga kupata pointi 10  kwa ikishinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja ikiwa nafasi ya kwanza, ambapo mshambuliaji huyo alifunga mabao matatu, huku Shaibu pia naye alitoa mchango mkubwa katika mafanikio hayo ya Yanga kwa mwezi huo hasa safu ya ulinzi na kuwa moja ya timu zenye ngome imara katika ligi msimu huu.

Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kuwa Kocha Bora wa Novemba akiwashinda Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda na Kaimu Kocha Mkuu wa Alliance FC, Gilbert Dadi alioingia nao fainali.

Zahera aliiongoza timu yake kupata pointi 10 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja, ambapo Yanga iliifunga Mwadui mabao 2-1 mjini Shinyanga, ikaifunga Kagera Sugar mabao 2-1 mjini Bukoba na pia iliifunga JKT Tanzania mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ilifungana bao 1-1 na Ndanda pia Dar es Salaam, hivyo Yanga kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.