Header Ads

Ukeketaji wamshtua mkuu wa mkoa wa manyaraWakati serikali na taasisi mbalimbali zikipinga juu ya ukeketaji mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amewataka watafiti hao kuthibitisha na kuonesha wanawake ambao wameeathirika mara baada ya kufanyiwa ukeketaji na siyo kuandika takwimu ambazo hazina uhalisia ndani yake.

Mbunge wa jimbo la Babati mjini  Paulina Gekul akashauri wataalamu wa mkoa watoe takwimu zinazoonyesha waliofariki kwa sababu ya kukeketwa.

Mkuu wa mkoa ameyasema hayo akiwa kwenye kikao cha ushauri cha mkoa mara baada ya Manyara kuelezwa kuongoza kitaifa juu ya suala la ukeketaji ambapo kwasasa inaelezwa kuwa Mangariba kubadili mfumo mzima wa ukeketaji ambapo kwa sasa hukeketa watoto wakiwa bado wachanga kwa kile kilichoelezwa kuwa wakiwa wadogo kidonda cha kukeketwa hupona kwa haraka kuliko mtoto akikomaa.

 “Unaweza ukawa unawaambia wananchi acheni kukeketa kumbe wanakuchora huyu anaongea unakuta watu wamezoea kufanya hivyo zaidi ya miaka 400 iliyopita wewe leo unakuja na utafiti wako uliofanya mwaka huu hawezi kuelewa, mimi nafikiri wataalamu watuletee elimu ya uelewa wa pamoja ilituweze kuwapelekea wananchi”alisema Mnyeti.

“ Mtafiti aliyefanya utafiti akagundua ukeketaji manyara unafanyika kwa kiwango cha juu tunataka atueleze ni wilaya gani au kijiji gani kata ipi na mtaa upi pia atueleze ni boma ipi alienda kufanya utafiti na akakuta wangapi wamekeketwa na atutajie majina yao vinginevyo hatutawaelewa, hawa watafiti wasituchafulie mkoa wetu kila siku kutuambia Manyara inaongoza kitaifa ukeketaji, tunataka takwimu halisi”alisisitiza Mnyeti.

Naye mbunge wa viti maalumu mkoa wa manyara martha umbula akaeleza kusikitishwa na taarifa zinazotolewa na taasisi mbalimbali juu ya mkoa wa manyara kuongoza kitaifa nakueleza kuwa yeye kama mbunge wa Manyara aliuliza swali la msingi bungeni ambalo lilikuwa likihoji ni wilaya gani na kijiji kipi kilichofanyia utafiti huo ili washirikiane kwa pamoja kutokomeza tatizo hilo lakini hakupewa majibu.

Kwa upande wake mganga mkuu mkoa wa Manyara Damas Kyera akaeleza kuwa madhara yatokanayo ni pamoja na kuathirika kisaikolojia pamoja na maambukizi ya magonjwa yatokanayo  na kushirikiana vifaa vinavyotumika kufanyia ukeketaji huo.

Aidha Dr.Kyera amesema asilimia 30 ya wanawake wanaofika kujifungua katika vituo vya afya wanaonekana wamekeketwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya afya,maendeleo ya Jamii jinsia wazee na Watoto,inaeleza kuwa kwa Manyara kiwango cha ukeketaji kipo kwa asilimia 58% .

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.