Header Ads

Wataalamu wa mifugo watakiwa kutumia tafiti


Wataalamu wa mifugo nchini wamesisitizwa kutumia tafiti mbalimbali kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili mifugo ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kiuchumi na kuboresha maisha ya wafugaji.

 Akifungua mkutano wa 36 wa mwaka wa Wataalam wa Masuala ya Mifugo Tanzania ulioandaliwa na Chama cha Veterinari Tanzania (TVA), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulika Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema sekta hiyo ni nyeti inayohitaji kuleta tija kwa wafugaji pamoja na kujikwamua kiuchumi.

 Alisema ni vyema wataalam hao kutumia tafiti mbalimbali zinazoleta tija ili kudhibiti magonjwa yatokanayo na mifugo na iendelee kuleta tija zaidi kwa wafugaji.

 “Lazima sasa mifugo hii ikaboreshwa zaidi ili kuinua uchumi badala ya wafugaji kutopata maendeleo hivyo ni vyema sasa wataalam kutoka vyuo vikuu kuhakikisha wanatatua changamoto za wafugaji na wao kujifunza zaidi mafunzo kwa vitendo”. Alisema Prof. Gabriel

 Prof. Gabriel alitoa rai kwa wataalam hao kuhakikisha wanatoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea sekta hiyo ili kuhakikisha pale wanapoenda kutoa huduma katika sekta hiyo wanatatua changamoto za mifugo.

 Alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na kwamba wizara ya mifugo na uvuvi imeweka dawati maalum la kuhakikisha wanashirikiana na sekta hiyo ili kutatua changamoto za mifugo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Veterinari Tanzania (TVA), Prof. Dominic Kambarage, alisema  ni vyema sasa wafugaji wakapewa elimu ya kutosha pamoja na upatikanaji wa chanjo za mifugo ili kudhibiti magonjwa pamoja na kupata masoko ya uhakika ili kila mtu anufaike na rasilimali hiyo.

 "Sekta ya mifugo ni sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi na Tanzania ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, hivyo mifugo hiyo ikitumika vyema itasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuongeza kipato, " alisema Prof. Kambarage

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.