Header Ads

Miss Algeria menye asili ya weusi akumbana na ubaguziMrembo aliyeshinda taji la mashindano ya ulimbwende wa Algeria hivi karibuni amelazimika kuwajibu wanaomkashifu kwa maneno ya kibaguzi kutokana na rangi ya ngozi yake.
"Sitarudi nyuma kwa sababu ya watu wanaonikosoa," Khadija Ben Hamou ameiambia mtandao wa habari nchiniAlgeria wa TSA.
Maneno ya kashfa kuhusu rangi yake nyeusi ya ngozi, pua na midomo yake yametapakaa kwenye mitandao ya Facebook na Twitter.
Raia wa Algeria wenye ngozi nyeusi hukabiliana na ubaguzi katika nchi hiyo iliyopo Afrika Kaskazini.

Mrembo huyo Bi Ben Hamou, anayetokea mkoa wa kusini wa Adrar, alisema kwamba anaona fahari ya utambulisho wake na kushinda mashindano hayo.
"Nimepata heshima kubwa na nimetimiza ndoto yangu, na ninajisikia nimepewa heshima kubwa na mkoa wa Adrar ninakotokea," amesema.
"Ninawashauri wasichana kutoka mkoani kwangu washiriki mashindano haya kama wanatamani," ameongeza.
Kwa mujibu wa jarida la mitindo Vogue, yeye ni mwanamke wa pili mweusi - baada ya Nassima Mokadem mwaka 2005 - kushinda mashindano hayo ya mwaka nchini humo.
Ben Hamou alishiriki mizunguko 20 kabla ya kuvaliswa taji la mlimbwende wa Algeria 2019 siku ya Jumamosi.
Wanaompinga wanadai kuwa yeye si taswira halisi ya uzuri wa Algeria, lakini pia amepata uungwaji mkono mkubwa kutoka baadhi ya watu mtandaoni.

Mlimbwende Ben Hamou ameiambia TSA, "usihukumu watu bila wao kujua, hakuna tofauti kati ya weupe na weusi."
Waandaaji wa mashindano ya Miss Algerie wamesema kuwa wamesikitishwa na "tabia ya ubaguzi wa rangi na maoni ya watu kadhaa kutokana na machapisho na picha za kutengenezwa".

Uzuri katika nchi ya Algeria na nchi nyengine za Afrika Kaskazini unahusishwa na rangi ya ngozi yako. Kadiri unavyoonekana kuwa mweupe machoni mwa watu wengi ndio unavyoonekana kuwa mzuri zaidi.
Hivyo wakati baadhi ya wananchi wa Algeria walipotambua kuwa mlimbwende anayeenda kuwatambulisha kimataifa ni mweusi, ilikuwa ni mshituko mkubwa kwao. Manyanyaso aliyoyapata Ben Hamou kutoka katika mitandao ya kijamii yalihusu rangi yake ya ngozi na wengine walimcheka umbile la pua, sura na midomo. Wapo waliofikia hatua ya kusema anaonekana kama mwanaume.
Wanawake weusi pia hubugudhiwa nchini Morroco, ni kuhusu rangi yao sanasana wakiwa wadogo.
Tatizo kuhusu kaskazini mwa Afrika ni kwamba unapata hisia kwamba watu wanao kunyanyapaa hawajui hata kama wanafanya ubaguzi wa rangi. Kinachoendelea kumtokea mlimwende huyo wa Algeria kinaweza kufumbua watu macho juu ya ubaguzi lakini ni vigumu kusema kwamba itabadilisha hali ya mambo.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.