Header Ads

Auawa Akiamulia Ugomvi wa Wanandoa Mke na Mume


MKAZI wa Lizaboni Manispa ya Songea mkoani Ruvuma, Mohammed Hamim, ameuawa kwa kupigwa na kipande cha bomba la chuma kichwani alipokuwa akiamulia ugomvi wa mume na mkeo ambao ni majirani zake.

Akizungumza na Nipashe jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tatu usiku katika mtaa wa Pacha Nne, kata ya Lizaboni .

Kamanda Mushy alisema siku hiyo ya tukio hilo, Hamim alikuwa amekwenda nyumbani kwa Soud Mdoka baada ya kusikia kelele zilizokuwa zikiashiria kuomba msaada na baada ya kufika, aliwakuta Mdoka na mke wake, Paulina Mlenga (35) wakiwa wanapigana.

Alisema baada ya kuona hivyo, Hamim alianza kuwaamulia jambo ambalo lilisababisha apigwe na kipande cha bomba la chuma kichwani na kumsababishia kifo papo hapo.

Mushy alisema Mdoka baada ya kubaini kuwa amemfanyia kitendo kibaya jirani yake kwa kumpiga na kufa papo hapo, alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Kutokana na kitendo hicho, Kamanda Mushy alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linamsaka Mdoka na akipatikana atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu mashtaka ya mauaji yanayomkabili.

Pia alisema mke wake, Paulina Mlenga, anashikiliwa na polisi katika jitihada za kumtafuta mume wake na mwili wa marehemu umeifadhiwa kwenywe chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea kwa uchunguzi

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.