Header Ads

Bidhaa za magendo zapigwa mnada Zanzibar


Na Thabit Madai 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepiga mnada bidhaa zote zilizokamatwa zikiwa zinasafirishwa
kwa magendo ikiwemo Sukari na Mafuta huku ikitarajia kupiga mnada Maboti na Majahazi yaliyokamatwa kwa makosa ya kusafirisha bidhaa za magendo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir alisema hatua hiyo ina lengo la kutaka kuona suala la magendo linakomeshwa kabisa.

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha suala la magendo linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria mpya ya ambayo inatoa adhabu kali kwa watendaji wote watakaopatikana wanajihusisha na vitendo hivyo.

Waziri Kheir alitoa maelezo hayo alipokuwa akijibu suali la nyongeza liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Ali Suleiman Haji, alietaka kujua mpango wa Serikali wa kupambana na watu wanaojihusisha na magendo nchini.

Alieleza kuwa Serikali imenunua vyombo vya kisasa kwa lengo la kupambana na watu wnaofanya magendo hasa wanaojitosa baharini baada ya kukamatwa.

Aliwatahadharisha wananchi kuacha vitendo hivyo kwani wanaweza kufilisika na kujijengea taswira mbaya kwa Serikali.    

Awali Naibu Waziri wa Wizara hiyo Shamata Shaame Khamis alisema hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, mali yote iliyokamatwa ilikuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 426 hivyo Serikali ingekosa zaidi ya shilingi milioni 76 za ushuru.

Aliyataja maeneo yanayoongoza kwa magendo kuwa ni pamoja na Kizimkazi, Uzi, bandari ya Nyamanzi na maeneo ya Kusini

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.