Kamishna Mkuu UNHCR aomba msaada wa kimataifa kwa Tanzania, inayohifadhi wakimbizi 330,000
Dar es Salaam, Februari 8, 2019; Kamishna
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani,
Filippo Grandi amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku nne nchini
Tanzania kwa kuomba uwekezaji katika ulinzi wa mazingira na maendeleo ya
kiuchumi katika maeneo ya Kaskazini-Magharibi mwa nchi ambako wakimbizi
takribani 330,000 wanahifadhiwa.
Ameitaja Tanzania kama “moja ya nchi muhimu zitoazo uhifadhi kwa wakimbizi Afrika,” Bw. Grandi ameelezea kuridhishwa kwake na hakikisho la serikali kwamba nchi itaendelea kuwa yenye ukarimu kwa wakimbizi.
Ameitaja Tanzania kama “moja ya nchi muhimu zitoazo uhifadhi kwa wakimbizi Afrika,” Bw. Grandi ameelezea kuridhishwa kwake na hakikisho la serikali kwamba nchi itaendelea kuwa yenye ukarimu kwa wakimbizi.
Katika
mkutano wake na Mheshimiwa Raisi, Dkt. John Joseph Magufuli, Bw. Grandi
ameipongeza Tanzania kwa utamaduni wake wa muda mrefu wa kuwakaribisha
wakimbizi wanaokimbia machafuko na mateso katika nchi zao, ikiwa ni
pamoja na kuwapa uraia watu 162,000 waliokimbia kutoka Burundi mwaka
1972. Amesema ukarimu wa Tanzania na Watanzania uliodumu kwa miongo
mingi kwa watu wanaotafuta hifadhi unastahili kutambuliwa kimataifa.
Ameahidi
kuendelea kukusanya misaada ya kibinadamu na ya maendeleo kwa nchi
mwenyeji, kwa lengo la kuimarisha usalama katika maeneo ya makambi na
kuendeleza miradi ya mazingira ikiwa ni pamoja na kutafuta nishati
mbadala wa kuni. Pia, walijadili wazo la kuanzisha mfumo wa kikanda
utakaojikita katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi wa nchi
za Burundi na Kongo.
Katika
kikao chake na maafisa wa serikali, Bw. Grandi alisisitiza kwamba
urejeshwaji wa wakimbizi wenye tija unatokea pale wakimbizi wanapoamini
kuwa ni salama kurudi makwao na wakipokea misaada muhimu utakaowawezesha
kujihudumia mara watakapofika katika nchi zao. Katika miaka miwili
iliyopita, wakimbizi 57,865 kutoka Burundi wamesaidiwa kurudi kwa hiari
kutoka Tanzania.
Hata
hivyo, baadhi ya wakimbizi wameripoti kuwa shinikizo kutoka kwa maafisa
wa serikali linalojumuisha kuzuiliwa kutembea maeneo mengine na
upatikanaji wa fursa za kuendesha maisha vimewafanya waamue kurudi
makwao. Bw. Grandi amesema kwenye mkutano wake kwamba UNHCR iko tayari
kufanya kazi pamoja na serikali katika kuwasaidia wale wote wanaoonyesha
utayari wa kurudi nyumbani lakini kwa uzoefu wake, baadhi ya vikwazo
vinaweza visiwe na manufaa na kwamba ni pale tu wakimbizi wanapoamini
kuwa hali ni salama kwenye nchi zao ndipo watakapochagua kurudi kwa
hiari yao.
“Katika
nchi za Kongo na Burundi bado kuna hali ya sintofahamu,” Bw. Grandi
amesema kwenye mkutano wake na vyombo vya habari kufuatia ziara yake
katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu, huku akisema
hata hivyo baadhi ya wakimbizi wako tayari kurudi na wanasaidiwa na
UNHCR. “Ni muhimu urejeshwaji ubaki kuwa jambo la hiari na kwamba hakuna
anayeshinikizwa kurudi.” Bw. Grandi ameomba msaada wa kimataifa ili
kuhakikisha kuwa wakimbizi wanaorudi kwa hiari wanaweza kuanza upya
maisha katika nchi zao za asili na kujitegemea, akisema msaada
unaotolewa sasa pamoja na fedha havitoshelezi mahitaji ya wale wanaorudi
Burundi.
Bw.
Grandi amerejelea Tanzania kama nchi imara katika kanda isiyo na
utulivu wa kisiasa na ameipongeza nchi kwa jukumu lake kama mtunza amani
wa kanda, akiuhimiza uongozi wa Tanzania kuendeleza jitihada za amani.
Katika mkutano wake Dar es Salaam na Rais mstaafu wa Tanzania,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ambaye hivi karibuni alikuwa
Mwezeshaji
mwakilishi wa Umoja wa Afrika ya Mashariki katika Mjadala wa Mazungumzo
ya Mchakato wa amani wa Burundi, Bw. Grandi alielezea matumaini yake
kuwa juhudi za usuluhishaji zitaendelea. Bw. Mkapa alionyesha wasiwasi
kuwa mchakato huo umesimama na, ingawa kuna hatua ilipigwa katika eneo
la usalama, kikwazo cha kisiasa kinabakia na majadiliano kati ya wadau
ndiyo njia pekee ya kumaliza mgogoro wa sasa na katika kuwezesha
uchaguzi huru, wa haki uliopangwa kufanyika mwaka 2020.
Asilimia
74 ya wakimbizi na watafuta hifadhi walioko Tanzania wanatoka Burundi,
na asilimia 26 nyingine wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wengi
wao wanaishi kwenye kambi karibu na maeneo ya mipaka, na wengi wao
wamekuwa hapo kwa miongo mingi sasa.
Bw.
Grandi aliisifu Tanzania kwa kuuunga mkono jitihada za Muungano wa
Pamoja wa Kimataifa kwa Wakimbizi ambao utawezesha kuomba msaada mkubwa
kutoka jumuiya za kimataifa kwa ajili ya kuzisaidia nchi wenyeji. Pia
inaomba uwezeshaji wa wakimbizi katika kujitegemea kwa lengo la kukuza
uchumi na kutoa fursa kwa wenyeji, alisema Bw. Grandi.
Wakati
wa ziara yake kwenye kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, mkimbizi kutoka
Kongo, Selemani Boaz, ambaye ni mfanyabiashara katika soko la pamoja
lililoko nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, alisema, “soko
linatusaidia kuwasiliana na kuonana na watu tofauti tofauti, hata kutoka
nje ya kambi, hasa Watanzania .... Tunapata kufahamiana na hii husaidia
kutuunganisha.” Bw. Grandi pia alisikia kutoka kwa wakimbizi kuwa soko
linawawezesha pia wakimbizi kupata vyakula vya aina mbalimbali, tofauti
na mgao wa chakula wa Shirika la Chakula Duniani (WFP).
No comments:
Post a Comment