Header Ads

Kamishna wa uhamiaji awataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama


Kamishna wa Uhamiaji Tanzania, Generali Anna Pita Makakala amewataka wananchi  kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini kutoa taarifa za kihalifu zinapotokezea ili kuweza kukabiliana nazo.

Ameyasema hayo katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Tunguu katika ziara ya kutembelea Ofisi za Uhamiaji za Mikoa ya Zanzibar ili kuona utendaji kazi na changamoto zinazokabili Ofisi hizo katika juhudi za kuimarisha hali ya utulivu na amani nchini.

General Anna aliwapongeza maafisa wa Uhamiaji wa Mikoa ya Kaskazini na Kusini Unguja  kwa kuimarisha ulinzi wa doria kwenye bandari zisizo rasmi katika juhudi za kupambana na wahamiaji haramu wanaojitokeza katika baadhi ya wakati katika bandari hizo.

Aliwaeleza maafisa hao kuwa Uhamiaji imepanga mikakati ya kudhibiti wahamiaji haramu kwa kuimarisha ulinzi sehemu za mipakani na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria za Uhamiaji Tanzania.

Nae Kamishna msaidizi wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Haji Abdallah amesema hali ya usalama katika Mkoa wake iko vizuri isipokuwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto waliochini ya miaka 18 vimekuwa vikitokea mara kwa mara lakini wamekuwa wakikabiliana navyo kwa juhudi kubwa ili kuviondosha.

Akizungumzia suala la makosa ya usalama barabarani alisema hali siyo mbaya sana na tokea kuanza mwaka huu 2019 ni ajali mbili tu zilizotokea ambapo moja ilisababisha kifo cha mtu  mmoja.

Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja Jumanne Tabarani Mzee amemueleza Kamishna wa Uhamiaji Tanzania kwamba wamejipanga vizuri katika kukabiliana na magendo hasa katika bandari zisizo rasmi.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili Unguja, Kamishna Uhamiaji Tanzania alitembelea Ofisi za Uhamiaji za Mikoa ya Kaskazini na Kusini, vituo vya uhamiaji na Bandari ndogo zilizomo ndani ya Mikoa hiyo

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.