Header Ads

Maambukizi ya ugonjwa wa Trachoma yapungua kwa asilimia 75


Maambukizi ya ugonjwa wa vikope (Trachoma) yameonekana kupungua kwa zaidi ya aslimia 75 katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokua hayapewi kipaumbele katika Ukumbi wa Hotel ya Morena jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema ugonjwa wa Vikope unawapata watu wa jamii ya kimasikini hasa wafugaji na pia jamii yenye changamoto ya upatikanaji wa maji safi. “Trachoma ni ugonjwa ambao kwa kiasi fulani unahusiana na umaskini na unawapata watu wa jamii ya wafugaji lakini pia wakiwa na changamoto ya upatikanaji wa maji”. Alisema Waziri Ummy.

Aidha, waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitano serikali imekua ikishirikiana na serikali ya Uingereza kupitia taasisi ya UK aid na Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust katika kuhakikisha wagonjwa wa Vikope wanafikiwa na kupata huduma za matibabu pamoja na kufanyiwa upasuaji kwa wale ambao wanakaribia kupata upofu.

Waziri Ummy amesema bado kuna changamoto ya maambukizi katika wilaya nane ambazo ni Mpwapwa, Chemba, Kalambo, Songwe, Ngorongoro, Longido, Kiteto, na Simanjiro.

Hata hivyo katika kipindi cha miaka mitano wagonjwa wa Trachoma waliofanyiwa upasuaji wamepungua kutoka 160,000 mwaka 2010 hadi wagonjwa 17,000 mpaka mwezi Oktoba 2018, ambapo inatajwa kuwa ni hatua kubwa katika mafanikio ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huu.

Waziri Ummy amesema serikali iko katika hatua nzuri ya kuhakikisha inatokomeza maambukizi mapya ya Trachoma kwa kuendelea kutoa dawa katika wilaya nane zilizotajwa na kuwafanyia upasuaji wagonjwa ambao wamefikia hatua ya kupata upofu.

Naye balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Cooke amesema serikali ya Uingereza kupitia taasisi ya Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust na shirika la SightServers itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kusaidia kutokomeza ugonjwa wa Trachoma nchini.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.