Header Ads

Ray C Afunguka Kuhusu Kuolewa, Kuzaa na Mzungu

Ray C Afunguka Kuhusu Kuolewa, Kuzaa na Mzungu
“NATAKA niwe na wewe milele, nataka tuwe na watoto baby, nataka tuishi wote pamoja…”

Hiyo ni sehemu ya mashairi matamu ya wimbo bora wa muda wote wa Na Wewe Milele ulioimbwa na mmoja wa wanamuziki ‘malejendari’ wa kike wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambayo sasa yanasadifu kinachoendelea kwenye maisha yake.Taarifa ikufikie kuwa, Ray C amechumbiwa na mtasha na kinachofuata ni kuolewa na kupata watoto kwa majaliwa ya Mola.

Katika mahojiano ‘exclusive’ na Gazeti la Risasi Mchanganyiko kwa njia ya simu akiwa London nchini Uingereza anakoishi kwa sasa, Ray C almaarufu Kiuno Bila Mfupa alifunguka yote, zaidi ikiwa ni juu ya kuolewa na kuzaa na Mzungu.

TETESI NYINGI

Kwa muda mrefu, kumekuwa na maswali mengi kutoka kwa mashabiki wake sehemu mbalimbali duniani, wakitaka kujua kinachoendelea kwenye maisha yake kwani hawamuoni majukwaani Bongo.

Mbali na hilo, pia mitandaoni kumekuwa na tetesi nyingi kuwa mwanadada huyo kwa sasa ana maisha mazuri mno huko London baada ya kuchumbiwa na mtasha.

Kufuatia mambo hayo kutopata uhakika, gazeti hili lilijipa ‘asainmenti’ ya kumtafuta Ray C na kummwagia maswali kama yote ambapo mambo yalikuwa hivi;HUYU HAPA RAY C

Risasi Mchanganyiko: Mambo vipi Rehema (Ray C)? Habari za kupotea?

Ray C: Poa, karibu.

Risasi Mchanganyiko (mwandishi anajitambulisha): Kwa muda mrefu umekuwa kimya na mashabiki wako wanatamani kujua kulikoni?

Ray C: Mimi nipo na nina kazi (nyimbo) ambazo nilipozitoa zilifanya vizuri sana na zinaendelea kufanya poa sana. Kama watakumbuka mwaka juzi niliachia Wimbo wa Umezima, mwaka jana nikaachia Hatuachani na Rogaroga hivyo si kweli kwamba nipo kimya. Mwaka huu watege sikio maana mambo mazuri yanakuja.


Risasi Mchanganyiko: Pamoja na kusikiliza nyimbo zako, lakini hawakuoni majukwaani kwenye matamasha mbalimbali hivyo wanasema wanamisi ile fleva yako ya Kiuno Bila Mfupa, wanauliza vipi?

Ray C: Ni kweli muda mwingi niko nje ya nchi kwenye shughuli zangu binafsi, lakini nikipata shoo huwa ninafanya. Kwa mfano wiki hii nina shoo Houston (Texas, Marekani). Hivyo shoo zipo tu na zikija za huko Bongo wataniona tu.

Risasi Mchanganyiko: Mashabiki wako wanajua upo Uingereza, lakini hawajui una projekti gani huko?Ray C: Ukiona nipo London, ujue nipo kwa fiancee (mchumba) wangu (amechumbiwa na Mzungu, raia wa Uingereza).

Risasi Mchanganyiko: Kuna hizi tetesi za mitandaoni kuwa umeolewa kwa siri huko na Mzungu, je, ni kweli?

Ray C: Ukweli ni kwamba sijaolewa, lakini nina mchumba ambaye tupo kwenye process (taratibu) za kufunga ndoa.Risasi Mchanganyiko: Wengine wanauliza hivi Ray C hutamani kuwa na watoto maana umri nao unakwenda na tayari una mchumba wa kueleweka?

Ray C: Natamani sana kumzalia mchumba wangu na nina mpango huo, sema acha niolewe kwanza kwani mtoto wa ndoa ana baraka zake.

Risasi Mchanganyiko: Wanaokuona mitandaoni wanasema umepungua vizuri, nini siri ya urembo na pia wanasema umekuwa mweupeee, kulikoni?Ray C: Hakuna siri yoyote zaidi ya mazoezi na kula vizuri. Siri ni kuzingatia mazoezi na kufuata dayati.

Risasi Mchanganyiko: Je, una jambo lolote ambalo ungependa ‘kushea’ na mashabiki wako popote walipo, lakini zaidi wa Bongo?

Ray C: Nimerudi rasmi kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva na hii ni kwa ajili ya mashabiki wangu tu hivyo ninawaomba wanipokee na kuendelea kunisapoti na mimi sitawaangusha.RAY C NI NANI?

Ray C aliyezaliwa Mei 15, 1982 mkoani Iringa ni mwimbaji wa R&B, Afro-Jazz na Taarab ambaye mkononi ana albamu nne za Mapenzi Yangu (2003), Na Wewe Milele (2004), Sogea Sogea (2006) na Touch Me (2008).

Ray C aliyesifika kwa kukata mauno alianza kujulikana baada ya kutoa nyimbo kadhaa kama vile, Sikuhitaji, Mapenzi Yangu, Na Wewe Milele, Ulinikataa na nyingine nyingi zilizompa umaarufu.

Awali alikuwa mtangazaji wa Radio East Africa kabla ya kwenda Clouds FM na hatimaye kuwa mwimbaji maarufu aliyeutingisha muziki wa Bongo Fleva.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.