Header Ads

Mvua zakatisha mawasiliano ya kata wilayani Nachingwea
Mvua zinazoendelea kunyesha katika kata za Kiegei, Kilimarondo na Matekwe wilayani Nachingwea na kuvunja kalavati ya mto Nanjihi zinasababisha adha kwa wananchi wa kata ya Kiegei wanaokwenda na kurudi Kilimarondo hadi Nachingwea.

Akizungumza na Muungwana Blog kutoka kijijini Kiegei Diwani wa kata ya Kiegei, Shaaban Madogo alisema baada ya kuvunjika kalavati ya mto Nanjihi kulikosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata hizo ,magari yanamalizia safari zake katika kijiji cha Kilimarondo badala ya Kiegei.

Amesema hali hiyo inasababisha adha kubwa kwa wananchi wanaoingia katika kata ya Kiegei na ambao wanatoka katika kata hiyo kwenda Kilimarondo hadi Nachingwea, huku nauli za bodaboda zikiwa zimepanda.

"Niliwataarifu TARURA(Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini) wakati kalavati hiyo ikiwa imekatika nusu,ilikuwa tarehe tatu mwezi huu. Hata hivyo tarehe kumi mwezi huu ilimalizika kuvunjika. Waliniambia wanatafuta gari ili waje kwasababu gari yao imeharibika,"alisema Madogo.

Diwani huyo alisema kwakuzingatia kwamba kituo cha afya kipo Kilimarondo amewahamasisha wananchi,wakiwamo wafanyabiashara waliopo kwenye kata hiyo wapeleke na kutandika magogo kwenye mto huo ili vyombo vya usafiri na watu waweze kupita kirahisi.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.