Header Ads

Serikali yajitosa kutatua mgogoro wa wawekezaji wa kilimo cha Kahawa


Serikali imeitaka Kampuni ya Tudeley Estates Limited  kutoka Uingereza iliyoingia mkataba na vyama vya Ushirika Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro vinavyojishughulisha na uwekezaji wa Kilimo cha Kahawa (Murososangi), kurudi nchini ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro uliosababishwa na kuibuka kwa mwekezaji mpya ambae mkataba wake haujulikani.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angela Kairuki walipofanya mkutano na Wawekezaji, Vyama vya Ushirika na Wadau wengine kuhusu mgogoro na Mwekezaji huyo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Mpango alisema kuwa, Vyama vya Ushirika vya Murososangi, viliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited ya nchini Uingereza ambapo washirika hao wenye mashamba eneo la Kibo na Kikafu  wilayani Hai, yenye ukubwa wa hekari 2054 walimpa Mwekezaji huyo ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka 1998.

Alisema kuwa baada ya mwekezaji  huyo, Bw. Conrad Legg, kuonesha nia ya kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua hisa bila  kuvishirikisha Vyama vya Ushirika vilivyoingia mkataba wa awali jambo lililosababisha sintofahamu kwa wana ushirika hao.

“Aliyeingia mkataba na Murososange, arudi nchini ili kutatua mgogoro huo ili kuona Wananchi wanawezaje kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi wenye mashamba hayo na pia mwekezaji”, alisema Dkt. Mpango.

Alisema Wanaushirika hao wanataka Mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa mkataba huo haujaisha muda wake hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji mpya wakati ule wa awali bado unaendelea.

Aidha, alisema kuwa mwekezaji mpya kutoka Ujerumanim Bw. Marcus Shiber,  alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji  na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake, madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila kupata muafaka na Vyama vya Ushirika jambo ambalo liliendelea kuleta mgogoro.

Dkt. Mpango alisema kuwa, wamepata maelezo kutoka pande zote na baadhi ya maelezo hayo yanahitaji ushauri wa kisheria hivyo tumeiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuyafanyia kazi mambo hayo ili kuweza kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, namna bora ya kumaliza mgogoro huo bila kuingizia Serikali hasara.

Aliwatahadharisha watendaji wakuu wa serikali kutotumia ubabe na vitisho kwa wawekezaji ili kutoharibu taswira ya taifa katika masuala ya uwekezaji unaopigiwa chapuo hivi sasa na Serikali ya Awamu ya Tano, ili kuvutia mitaji, mapato ya serikali, ajira kwa vijana na kuvutia teknolojia za kisasa kwa maendeleo ya Taifa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, alisema kuwa kutokana na mgogoro huo wa kiuwekezaji akaunti za Mwekezaji mpya kutoka Ujerumani ikiwemo ya Kampuni ya Kuza Afrika inayojishughulisha na kilimo cha parachichi Mkoani Mbeya ilifungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhusiana na masualaya kodi, jambo lililosababisha baadhi ya shughuli za Mwekezaji huyo kukwama.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.