Header Ads

Tanzania yashiriki mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika


Tanzania imeshiriki katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Mkutano huo, unahudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mawaziri wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji na Mawaziri wa Fedha pamoja nchi 16 wanachama wa SADC ambapo Tanzania inawakilishwa katika mkutano huu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.);  Waziri wa Viwanda na  Biashara, Mhe. George Kakunda (Mb.); na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.).

Masuala yanayojadiliwa katika mkutano huu ni pamoja na  Taarifa ya Utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Visiwa vya Komoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha chuo cha Uhawilishwaji cha SADC (SADC  University of Transformation).

Masuala mengine yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huu ni pamoja  na; Uendelezaji wa viwanda katika kanda; Utekelezaji wa Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano; Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa Afrika(AU); na Majadiliano ya Ubia Mpya Baina ya Nchi za Kundi la Afrika, Carribean na Pasifiki (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU), baada ya mkataba wa Cotonou kumalizika mwaka 2020.

Mkutano huu umetanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu pamoja na maafisa
waandamizi  uliofanyika kuanzia tarehe 11 – 14 Machi, 2019, Windhoek.

Namibia. Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.