Header Ads

Zanzibar kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani

 

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said amesema Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa  Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) ili kukuza na kuimarisha teknolojia ya utumiaji wa mionzi.
Simai ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 15, katika mkutano wa pamoja na ujumbe wa IAEA, Kanda ya Afrika.
“Zanzibar Bado iko chini katika matumizi ya teknolojia ya mionzi, hivyo tunaomba ujumbe huu kuunganisha nguvu na Wizara ya Elimu kupitia Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili nao waweze kutoa elimu kuhusiana na matumizi ya teknolojia ya mionzi,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa IAEA, Kanda ya Afrika Profesa Shaukati Abdulrazak, amesema malengo hasa ya IAEA ni kutumia teknolojia katika uzalishaji wa vyakula, kuondoa wadudu waharibifu wa mazao na kupambana na maradhi ya saratani.
Aidha, amesema IAEA iko tayari kuwajengea uwezo Wazanzibar ili waweze kutumia teknolojia hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo zaidi.
“Lengo la teknolojia hiyo ni kuhakikisha kila chakula ni salama kwa matumizi ya kibinadamu lakini pia tutaendeleza ushirikiano ili kuhakikisha Zanzibar nayo inapata kifaa cha kupimia maradhi ya saratani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala, amesema kazi ya majaribio ya mwanzo ya shirika hilo la Zanzibar ni kuhakikisha hakuna kabisa wadudu wa mbung’o, zoezi ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Ushirikiano mzuri ndiyo utakaosababisha Wazanzibar kuendelea mbele kiteknolojia,” amesema Profesa Busagala.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.