Header Ads

Majaliwa -Serikali imeshahakiki madai ya wakandarasi waliotekeleza miradi ya maj


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi sasa, Serikali imeshahakiki madai ya wakandarasi waliotekeleza miradi ya maji nchini na imewalipa shilingi bilioni 138.

“Hivi karibuni tutalipa fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 44. Ninaielekeza Wizara husika ihakikishe kuwa watendaji wa Serikali wanafuatilia ufanisi wa wakandarasi na wajiridhishe kuwa wakati wote unakuwa wa kiwango cha kuridhisha,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alisema wakati wa michango yao, Waheshimiwa Wabunge walizungumzia upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na baadhi yao walikosoa utekelezaji na ubora duni wa baadhi ya miradi ya maji. Alisema wengine walionesha kutoridhishwa na utekelezaji huo kwani baadhi ya maeneo hayajafikiwa na miradi hiyo.

Waziri Mkuu alisema licha ya changamoto hizo, Serikali inaendelea na usambazaji wa maji, na itachukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inayotekelezwa, inatoa matokeo yaliyokusudiwa.

“Kwa kuanzia, Mheshimiwa Rais aliunda tume maalum ili kupitia, kufanya tathmini na kutoa mapendekezo juu ya hatua za haraka zinazostahili kuchukuliwa, kwa lengo la kuhakikisha thamani ya fedha kwa miradi hiyo inapatikana na kuleta tija,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema changamoto nyingine katika eneo la maji ni uharibifu wa mazingira ambao umeshika kasi kubwa na kwamba hatua za haraka hazina budi kuchukuliwa ili kuiepusha nchi na janga la ukame.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.