Header Ads

Mariam kuhamishiwa katika Hospitali ya Ocean Road


Baada ya Mariam Rajab Juma (25), mkazi wa Singinda kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua, wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameshauri ahamishiwe Hospitali ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Wiki iliyopita Mariam alifikishwa Muhimbili akitokea mkoani Singida na kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua katika kidonda kilichopo sehemu ya bega la mkono wake wa kulia.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Muhimbili, Dkt. Ibrahim Mkoma amesema Mariam ataanza matibabu rasmi katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na kwamba baada ya kumaliza matibabu atarejeshwa Muhimbili kuendelea matibabu zaidi.

Dkt. Mkoma amefafanua Mariam atahamishiwa Hospitali ya Saratani ya Ocean kwa kuwa kuna baadhi huduma za matibabu ambazo anapaswa kupatiwa katika hospitali hiyo kutokana na ugonjwa unaomsumbua.

Daktari alipoulizwa kuhusu ugonjwa unaomsumbua Mariam, Dkt. Mkoma amesema suala la ugonjwa ni siri ya mgonjwa na wataalam wa hospitali na kwamba taratibu za hazimruhusu kuweka wazi  aina ya ugonjwa unaomsumbua mgonjwa.

Naye Mariam amesema amefurahishwa na huduma nzuri ya matibabu aliyopatiwa na walaam wa Muhimbili kwani tangu alipofikishwa hapa amekuwa akihudumiwa vizuri.

“Hivi sasa naendelea vizuri, tangu nimekuja Muhimbili naendelea vizuri. Kabla sijafika Muhimbili nilikuwa siwezi kutembea vizuri lakini sasa naweza kutembea vizuri,” amesema Mariam.

Mariam alifanyiwa vipimo vya CT-scan ya kifua na kichwa, Ultrasound pamoja na vipimo mbalimbali vya damu ambavyo vimesaidia kubaini ugonjwa unaomsumbua Mariam.

Dkt. Mkoma amesema kidonda kilichopo sehemu ya mgongo wa Mariam ni kidonda sugu ambacho kilihitaji kufanyiwa vipimo mbalimbali kubaini ugonjwa unaomsumbua.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.