Header Ads

Mwanafunzi auwawa kikatili kwa kukatwa na panga shingoni


Mwanafunzi wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Mbambua Kata ya Lembeni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, Sarafina William (8), ameuawa kikatili kwa kukatwa panga shingoni akiwa amelala kitandani na mama yake mzazi

Hata hivyo, mama mzazi wa marehemu hakujeruhiwa na waliotekeleza mauaji hayo.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah, zinaeleza watu watatu ambao hawakujulikana ndio waliotekeleza mauaji hayo usiku wa manane wa kuamkia Jumapili.

Inadaiwa mama mzazi wa mtoto huyo, Salome William, akiwa amelala na mwanae nyumbani kwake, ghafla waliona mwanga na wakati wakijiuliza mwanga huo unatoka wapi, ndipo watu hao watatu walipoingia ndani na kumpiga panga shingoni mtoto huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, watu hao walimkata na panga mtoto huyo shingoni upande wa kushoto na kumsababishia jeraha kubwa, ambalo wakati anakimbizwa Hospitali ya Rufani ya KCMC, alifikwa na mauti njiani.

“Mtoto huyo kutokana na jeraha kubwa alilokuwa amelipata shingoni, hakuweza kufika Hospitali ya KCMC, badala yake alifia njiani, na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kusubiri uchunguzi wa kitabibu,” alieleza Kamanda Issah.

Aidha, Kamanda Issah alisema jeshi hilo linamshikilia mama mmoja (jina linahifadhiwa), kuhusiana na tukio hilo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na tukio hilo.

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.