Header Ads

Upelelezi kesi ya kina Tenga wakamilika baada ya mwaka mmoja na miezi minne


UPANDE wa mashtaka umekamilisha upelelezi katika kesi inayowakabili vigogo wa Kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwamo Wakili Dk. Ringo Tenga.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa Fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.
Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, alidai mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Mwita alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na ofisi ya mashtaka inaandaa nyaraka ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.
“Upande wa mashtaka tumekamilisha upelelezi dhidi ya washtakiwa wa Kampuni ya Six Telecoms Limited, tunaandaa nyaraka ya kesi ili ianze kusikilizwa,” alieleza Mwita.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17, mwaka huu itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka lao kutokuwa na dhamana.
Washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 20, 2017 wanakabiliwa na mashtaka sita likiwamo la utakatishaji fedha na hivyo kukosa dhamana hadi sasa.
Katika kesi ya msingi, Dk. Ringo, ambaye ni Mkurugenzi na Mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadai kuwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola 0.25 za Marekani kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.
Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola 3,282,741.12 za Marekani kwa TCRA kama malipo ya mapato.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola 466,010.07 za Marekani kwa TCRA.
Katika shtaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola 3,282,741.12 za Marekani wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.

Pia washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola 3,748,751.22 za Marekani (sawa na Sh bilioni nane).

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.